BALAA zito! Siku 13 baada ya kifo cha  mwanamuziki wa kizazi kipya, Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwair’, ripoti ya daktari inayoeleza sababu halisi ya kifo chake bado utata mtupu kwani haijawekwa wazi, hivyo kuwafanya wengi kuendelea kuamini uvumi.
 
Dawa za kulevya.
Kuhusu uvumi, vitu viwili vinavyotajwa sana ni ama kifo chake kilisababishwa na kuchanganya madawa ya kulevya pamoja na vilevi vingine, hivyo kutengeneza sumu iliyomuua au alibeba mzigo wa unga tumboni ambao ulimchachia na kumtanguliza mbele ya haki.
Huku tukisubiri ripoti hiyo kuwekwa wazi, Uwazi lipo kwenye wakati mzuri kueleza kinagaubaga jinsi wasanii wa Kitanzania walivyogeuzwa makuli wa kubeba mizigo ya madawa ya kulevya tumboni na kusafirisha kwenda nchi mbalimbali.
Habari zinaeleza kuwa wasanii mbalimbali nchini, wameingia kwenye mkumbo wa kusafirisha unga tumboni kutokana tamaa ya utajiri na wakati mwingine ni baada ya kuona maisha yao ya kimuziki hayawaendei vizuri.
Kutokana na kuingia kwenye biashara hiyo, wasanii hao hususan wanamuziki, hutambuliwa zaidi kwa jina maarufu la punda, kwa tafsiri kwamba wao ni sawa na mnyama huyo ambaye kazi yake kubwa ni kubeba mizigo ya binadamu.
Hoja kuhusu jina hilo ni kwamba wanaobeba madawa ya kulevya tumboni, wanajishusha thamani sawa na punda, kwani binadamu ni wale matajiri wanaowabebesha mizigo hiyo.
 
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
USHUHUDA WA SUGU
Ukweli wa jinsi matajiri wauza unga wanavyowatumia wanamuziki wa Kitanzania kama punda, unapewa nguvu na ushuhuda aliowahi kuutoa Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Mbunge huyo ambaye anapewa heshima kwamba ni mmoja wa waasisi wa Bongo Fleva, alimweleza mwandishi wetu kuwa kabla hajawa memba wa jumba hilo la kutunga sheria, aliwahi kufuatwa na wauza unga kumshawishi awe anabeba mzigo kwenda nao nje ya nchi.
“Jamaa waliniambia kwa sababu mimi nasafirisafiri sana, passport (hati ya kusafiria) yangu itakuwa imeshagongwagongwa sana, kwa hiyo ni rahisi kwenda nchi tofautitofauti kwa urahisi, kwa hiyo wakataka niwe nabeba unga.
“Kigezo cha pili waliona kwa sababu mimi ni mwanamuziki, kwa hiyo ni rahisi watu kuamini ziara zangu ni za kimuziki. Nilikataa, niliwaambia siwezi kufanya biashara hiyo kabisa,” alisema Sugu.
Mwaka 2011, mbunge huyo aliwahi kugusia hilo, wakati akitoa hoja kuchangia bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwa serikali ni lazima iwasaidie wanamuziki wa Kitanzania kwa sababu wanaibiwa sana, hivyo kuwafanya vijana kuona kimbilio rahisi la kutajirika ni kuuza madawa ya kulevya.
“Mheshimiwa spika, serikali isifanye ili kijana wa Kitanzania afanikiwe lazima auze unga, madawa ya kulevya,” alisema Sugu na kueleza mfano huo wa jinsi alivyofuatwa kushawishiwa na matajiri wa unga ili naye awe punda.
 
Jack Patrick.
PUNDA HULIPWA DOLA 3000 MPAKA 5000
Kwa mujibu wa mwanamuziki maarufu wa dansi nchini (jina tunalo), kwa wastani punda hulipwa fedha kulingana na umaarufu wake, kwa kuangalia kiwango cha mzigo anaobeba, vilevile nchi anayopeleka.
“Mara nyingi watu wanalipwa dola 3000 (shilingi 4,800,000) mpaka dola 5000 (shilingi 8,000,000). Binafsi nilishabeba madawa kutoka hapa Tanzania kwenda China, Botswana na Afrika Kusini, kila nilipofikisha mzigo nililipwa dola 5000,” alisema mwanamuziki huyo na kuongeza:
“Kuna kipindi nilinogewa, nikawa sijishughulishi sana na muziki, kila mara nipo safarini nakwenda kupeleka mzigo, nikirudi nipo vizuri na dola 5000 zangu. Hivi sasa nimeacha baada ya watu wangu wa karibu kunishauri na kunieleza kwa mapana hatari inayoweza kunipata.”
MTINDO WA SASA
Utafiti wa siku za hivi karibuni, umepata jawabu kwamba wauza unga wengi, wanawatumia wanamuziki na wasanii mbalimbali kusafirisha mizigo kwa sababu kwao ni rahisi kugongewa visa katika balozi za nchi wanazokusudia kwenda.
“Kule inaweza kuandaliwa shoo ya uongo na kweli, wewe unasafiri kwamba unakwenda kwenye hiyo shoo lakini kumbe ni utapeli mtupu. Kule hauendi kama mwanamuziki, isipokuwa ni punda tu,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza:
“Fikiria mtu unakwenda kwenye shoo halafu ukumbini wanaingia watu 40, halafu huyo mwandaaji anakulipa fedha zako vizuri, unalala hoteli nzuri, ukumbi analipa, kodi anatoa. Hii biashara ya madawa ya kulevya ina siri kubwa.
 
Khaleed Mohamed ‘TID’.
“Kinachosikitisha kwa wanamuziki wenzetu ni kwamba hawajitambui. Watu wanakufa jamani, kukubali kusafirisha madawa tumboni ni sawa kujiweka katikati ya uhai na kifo. Zile dawa zikipata joto tumboni huponi. Ukijisahau na kunywa kitu cha moto ni kifo.”
Mtoa habari huyo aliendelea kubainisha kuwa wanamuziki wa Kitanzania wengi wanakuwa nchini bila kazi mpaka wanakumbwa na hali ngumu ya uchumi kutokana na kutopata shoo za kutosha, hivyo kuwawia rahisi kukubali ofa ya kubeba madawa ya kulevya tumboni kwenda nchi mbalimbali.
“Hivi sasa kuna wimbi kubwa. Watakwenda hivyo ila baadaye madawa hufeli tu. Naamini itafika wakati tutashuhudia vifo vingi vya wanamuziki wetu. Mungu akiniweka hai nitasema, kwani nawajua wanamuziki wengi punda,” alisema.
Aidha, mtoa habari huyo aliwataja wanamuziki sita nchini ambao aliwataja moja kwa moja kuwa wanajishughulisha na usafirishaji wa madawa ya kulevya lakini majina yao tunayahifadhi kwa sasa.
 
Ambwene Yesayah ‘AY’.
MWANAMUZIKI ALIVYOMSHAWISHI MFANYABIASHARA
Kuna mwanamuziki (jina kapuni) ambaye hivi karibuni alirejea nchini baada ya kupata matatizo akiwa nje ya nchi, aliwahi kumshawishi mfanyabiashara mmoja aingie kwenye biashara ya madawa ya kulevya halafu yeye atakuwa anabeba.

Mfanyabiashara huyo (naye jina kapuni), alisema: “Nilishangaa yule dogo ananiambia yeye yupo tayari kubeba mzigo kusafirisha kwenda Afrika Kusini na nchi nyingine za Kusini ya Afrika.

“Aliniambia yeye ameshaweza kubeba madawa ya wafanyabiashara wengine na wakapata faida kubwa. Aliniambia faida ni mara mbili kwa asilimia 100. Nilimjibu siwezi kufanya hiyo biashara, baadaye akiwa huko alipata matatizo na hivi sasa yupo hapa nchini.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top