Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma jana, baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka katika eneo la Area ’E’ juzi usiku.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya kupigwa na watu wasiojulikana wakati akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge juzi.
Tukio la kuvamiwa na kupigwa kwa mbunge huyo, lilitokea saa 2.30 usiku wakati akirejea nyumbani kwake eneo la Area ‘E’ karibu na hoteli maarufu ya Summit.
Kwa mujibu wa Machali, watu hao ambao idadi yao haikujulikana, walimsimamisha akiwa mita chache kabla ya kuingia nyumbani kwake akiwa na gari yake ndipo wakaanza kumrushia maneno makali na kumtaka ashuke ndani ya gari.
“Sikuweza kuwafahamu na idadi yao sikuipata mara moja, lakini wameniumiza sehemu mbalimbali za mwili na hasa katika mguu wangu wa kulia sehemu ya paja na sehemu ya pua kama mnavyoona,”alisema Machali.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Chama cha NCCR –Mageuzi James Mbatia, alisema ni tukio baya na ambalo limeonyesha kulikuwa na makusudi maalumu ya kufanya hivyo.
“Ni mapema kueleza tukio hilo kwa sasa, lakini kwa mazingira ilivyotokea inatia mashaka makubwa na kweli tuwashukuru vijana wa CBE ambao waliyatoa maisha yao na kuamua kumsaidia vinginevyo wale walikuwa na nia mbaya,”alisema Mbatia.
Hata hivyo, alisema kuwa hali aliyokuwa nayo jana Machali ilikuwa afadhali ukilinganisha na alivyokuwa juzi wakati anapelekwa hospitalini, ambapo alimkuta akiwa amelowa damu mwili mzima kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu hata kumtambua.
Alipotakiwa kueleza kama tukio hilo linaweza kuwa na uhusiano na masuala ya kisiasa, alisema ni mapema kulizungumzia jambo hilo lakini akataka polisi waachiwe kwanza wafanye kazi yao kwani tangu juzi walitoa ushirikiano mkubwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Nassoro Mzee, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walimpokea Machali juzi majira ya saa 5:00 usiku na kuwa hadi jana alikuwa akiendelea vizuri.
Wabunge na viongozi wa Serikali jana walikuwa wakimiminika Hospitali ya Dodoma kumjulia hali, ambapo kwa jana asubuhi alikuwepo Mbunge Albart Ntabalima (Manyovu-CCM), Mbunge wa Kasulu Vijijini Zaituni Buyogela (NCCR- Mageuzi) ambaye tangu juzi usiku walikuwa wameambatana na Mbatia hadi polisi na hospitali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo hadi jana alisema tayari Polisi ilikuwa inawashikiliwa watu wawili wakihusishwa na tukio hilo.
Kamanda Misime aliwataja watu hao ambao alisema ni vibaka kuwa ni Jeremia Mkude (18) na Charles Chikumbili (22) ambapo walikamatwa na misokoto ya bangi na polisi inaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wawili.
Miongoni mwa waliokamatwa, mmoja Mkude alikamatwa akiwa na jeraha usoni ambalo lilitokana na kipigo kutoka kwa watu waliokuwa wakimsaidia Machali.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoa Dodoma linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumvamia na kumshambulia Mbunge Machali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo saa 1:00 jioni katika eneo la Area ‘E’ katika Manispaa ya Dodoma wakati akirejea nyumbani kwake.
“Alikutana na vijana wanne waliokuwa wamesimama katikati ya barabara akapiga honi lakini hawakupisha. Aliamua kuwauliza “Jamani mnasimama katikati ya barabara si nitawagonga?” Nao wakamjibu: “Wewe si unajifanya mtoto wa Mbunge, tutakupiga sasa”. Alisisitiza Kamanda Misime.
Kamanda Misime alisema mheshimiwa alipojaribu kupita vijana hao walipiga gari lake.
kitu ambacho kilimfanya ashuke ili atazame kama gari hilo limepata uharibifu wowote, ndipo vijana hao wakaanza kumshambulia kwa ngumi na mateke huku naye akijitahidi kujihami.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema askari walipowafanyia upekuzi watuhumiwa usiku huo wa manane walikutwa na misokoto miwili ya bangi.
 Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top