Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.

WAKATI Chadema wakikishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa inakihujumu, tuhuma nyingine nzito zimeibuliwa dhidi yake. Tuhuma hizo ni zile za mipango ya mauaji, ambako CCM kinadai kuwa kimebaini mpango wa siri unaoratibiwa na chama hicho kwa kuwahusisha askari Polisi na wananchi wa kawaida.

Hii si mara ya kwanza kwa vyama hivyo viwili vyenye upinzani mkubwa nchini kushutumiana hadharani juu ya tuhuma nzito kama hizo. Wakati CCM ikidai kuwa na ushahidi juu ya tuhuma za sasa, Chadema wamekuwa wakidai kuwa tuhuma kama hizo na nyingine ni mpango wa kutaka kukidhoofisha baada ya kuona kuwa ni tishio kwake.

Jana Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye, aliibua tuhuma nyingine nzito alizodai kuwa na ushahidi nazo dhidi ya Chadema mbele ya mamia ya wananchi aliokuwa akiwahutubia mjini Makambako na vitongoji vyake.

Katika mkutano huo, Nape alisema kuwa kumekuwa na mipango inayoratibiwa na CHADEMA kwa takribani mwezi mmoja sasa ya kufanya maandamano ambayo yataambatana na mauaji dhidi ya askari Polisi na wananchi wa mji huo na maeneo tofauti.

Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kuwa CCM imedhamiria kukishughulikia CHADEMA dhidi ya tuhuma hizo, Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, anaelezwa kupanga kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, mkoani Ruvuma kuangalia jinsi ya kushughulikia tuhuma hizo.

Nape akizungumza na wananchi hao, alidai kuwa mpango huo unawahusisha viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho cha upinzani.

“Ninapenda kuweka wazi jambo moja kwa mujibu wa taarifa za siri ambazo CCM imezinasa kutoka ndani ya Chadema, ni kwamba hivi sasa chama hiki kipo katika mikakati ya kufanya maandamano katika miji minne, ikiwemo Makambako.

“Lengo la maandamano hayo ni kuibua vurugu zitakazosababisha mauaji dhidi ya askari Polisi na raia wa kawaida, ili kutafuta umaarufu wao ambao umeanza kupungua kwa siku za hivi karibuni.

“CCM inapenda kuwaambia Watanzania popote pale walipo, wajue kuwa CHADEMA si chama cha siasa, bali ni genge la watu ambalo limejikusanya kwa lengo la kuua na kung’oa kucha watu. CCM haiko tayari kuona nchi inaingia katika shimo la mauaji ya kupanga hata kidogo.

“Kwa wiki moja sasa wamekuwa wakichagua miji ya kufanya maandamano yao ambayo yataambatana na mauaji na wamepanga kufanya katika miji ya Makambako, Songea pamoja na miji ya Ilula wilayani Kilolo pamoja na mji wa Ruaha, wilayani Kilombero,” alisema Nape, huku akishangiliwa na umati wa wananchi katika mkutano huo.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, alisema kwa muda mrefu chama chake kimekuwa kimya na kuacha vyombo vya dola vifanye kazi yake, hasa kwa watu ambao wamekuwa wakitaka kulitumbukiza taifa katika machafuko kwa kivuli cha siasa.

Alisema kutokana na hali hiyo, chama chake hakitakuwa tayari kuona kile alichodai kuwa mauaji yakitokea tena nchini, kama ilivyokuwa katika miji ya Arusha, Morogoro na Iringa.

“Ni wazi siku tatu kabla ya maandamano ya Morogoro yaliyosababisha kifo cha kijana mmachinga asiye na hatia, CCM ilijitokeza mbele ya umma wa Watanzania na kuwaambia kuwa kuna mipango ya mauaji inayopangwa na Chadema kwa kutoa watu jijini Dar es Salaam.

“Ilipotimu siku hiyo walifanya hivyo kwa kutoa magari kila kona ya jiji la Dar es Salaam na kwenda kuwaingiza vijana maskini wa Morogoro katika maandamano ambayo yalipigwa marufuku na Polisi.

“Haikupita muda alikufa kijana wa Kitanzania bila hatia, huku Mbowe na babu Slaa wakiwa Dar es Salaam wakiendelea na kazi zao, huku wakifanya mashauri na familia zao. Kama wao kweli wana uchungu na nchi hii, kwa nini hatuwaoni wakiwa mbele ya maandamano,” alisema Nape.

Kutokana hilo Nape, alisema kuwa moja ya kazi anayoifanya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa sasa ni kwenda mjini Songea ambako atafanya kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kumueleza juu ya mipango hiyo michafu inayolenga kuharibu sifa ya Tanzania.

Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, MTANZANIA Jumapili ilimtafuta Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa ili atoe ufafanuzi wa shutuma hizo, lakini simu yake iliita bila majibu, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake hiyo ya kiganjani pia hakujibu.

Alipotafutwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, naye hakujibu chochote.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top