Mandela na Winnie , katika siku za furaha
Mke wa zamani wa Nelson Mandela, Winnie amewasili katika hospitali
nchini Afrika Kusini, ambako inaaminiwa rais huyo mstaafu anaendelea
kupokea matibabu kwa ugonjwa wa homa ya mapafu.
Mtoto wao wa kike Zenani (Mandela - Dlamini) pia
amerejea nchini Afrika Kusini kutoka Argentina ambako anahudumu kama
balozi wa Afrika Kusini, ili awe na babake.
Bwana
Mandela, mwenye umri wa miaka 94, alipelekwa hospitalini mapema
Jumamosi , ikiwa ni mara ya tatu kulazwa hospitalini mwaka huu.
Kwa mujibu wa duru za urais, Mandela amekuwa
akiugua kwa muda mjini Johannesburg baada ya kukumbwa tena na ugonjwa wa
mapafu. Msemaji wa serikali Mac Maharaj amesema kuwa maafisa katika
hospitali wanataka kudhibiti idadi ya watu wanaozuru hospitali hiyo ili
wampunguzie bwana Mandela usumbufu.
Alilazwa hospitalini baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi mnamo Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa za urais, Rais
Jacob Zuma, amerejelea wito wake kwa watu nchini Afrika Kusini kumuombea
Madiba wakati huu anapougua.
Lakini mwandishi wa BBC mjini Pretoria, Karen
Allen, anasema kuwa kuna matumaini madogo kuwa Mandela aliyeongoza vita
dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, huenda akapona.
Anasema kuwa wengi walipata matumani baada ya
bintiye Mandela Zindzi, kusema kuwa babake yuko salama na kuwa
anaendelea kupata nafuu.
Mkewe Mandela Graca Machel, alifutilia mbali, ziara yake mjini London Jumamosi ili kuwa kando ya mumewe.
Mandela alikuwa Rais wa Afrika Kusini kati ya mwaka 1994 hadi 1999.
Alifungwa jela miaka 27 na anaaminika kuwahi
kuugua ugonjwa wa mapafu alipokuwa akifanyishwa kazi ngumu katika
machimbo ya mawe akiwa jela.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment