Rais Jakaya Kikwete.

MAANDAMANO makubwa ya kutaka Rais Jakaya Kikwete asikilize kilio cha wakazi wa Mtwara na Lindi wanaopinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam yanaandaliwa.

Baadhi ya wakazi wa Lindi na Mtwara kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF), Juni 29 mwaka huu wanatarajia kufanya maandamano hayo kutoka makao makuu ya CUF Buguruni hadi Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Maandamano hayo pia yatakuwa na lengo la kumtaka Rais Kikwete awang’oe madarakani mawaziri watatu ambao ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Emanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani).

Wakizungumza katika mkutano wa kongamano la gesi lililowakutanisha wakazi wa Lindi na Mtwara, lililofanyika jana jijini Dar es salaam katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF, baadhi ya wakazi hao walisema wamechoshwa na ahadi za serikali.

Walisema wanaamua kufanya maandamano kwenda Ikulu ili kilio chao kimfikie Rais Kikwete ambaye kama hatakisikiliza asitarajie wananchi watarudi nyuma kutetea rasilimali zilizoko mikoani mwao.

Walibainisha kuwa vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara ni ishara ya kuchoshwa na mgawanyo wa rasilimali unaofanywa na serikali ambayo hivi sasa badala ya kuufikiria mkoa wa Mtwara unahangaika kujenga bomba la gesi kutoka mkoani humo.

Lipumba aanza
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara zimesababishwa na serikali ya CCM iliyopuuza kilio cha umaskini cha wakazi cha mkoa huo.

Alisema serikali imeanza kushtuka na kwenda kuweka msingi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji baada ya machafuko na upinzani kutoka kwa wananchi.

Alibainisha kuwa nguvu na kuwaziba midomo wanasiasa, wananchi na wanaharakati kamwe hazitoisaidia serikali kutatua mzozo huo unaoonekana kuutikisa utawala wa Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa watu wa Mtwara na Lindi wamekosa mahali na fursa za kuonana na viongozi wao kuzungumzia suala la gesi na matokeo yake imesababisha vurugu, manyanyaso kutoka kwa polisi waliokwenda kutuliza ghasia.

Profesa Lipumba alisema serikali inaeneza propaganda za uongo kwamba wananchi wa Mtwara hawataki Watanzania wengine wafaidi rasilimali zinazotoka katika mkoa huo.

Alisema wananchi wanataka maendeleo yaanzie katika mkoa huo kutokana na rasilimali zilizopo ndani yake ikiwemo kujengwa kiwanda cha mbolea na kiwanda cha kufua umeme wa MW 300 kama ahadi ya serikali ya mwaka 2011 inavyoeleza.

Aliongeza kuwa serikali katika ahadi zake miaka miwili iliyopita iliwaeleza wananchi wa Mtwara kwamba ingejenga kiwanda cha mbolea na kujenga kiwanda cha kufua gesi ambayo ingezalisha umeme wa MW 300 kisha uunganishwe kwenye gridi ya taifa lakini mipango hiyo haikufanyika.

Alisisitiza kwamba endapo mipango ya serikali iliyoainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ingetekelezwa hakuna vurugu wala matatizo ambayo yangejitokeza.

Alisema wananchi wanaoishi mikoa ya kusini wanadharaulika na kuonekana hawastahili kupata haki kama watu wa mikoa mingine na kwamba hali hiyo imewafanya wachoke na kufanya matendo ambayo yataaonyesha kuchoshwa na kuhitaji mabadiliko.

Wakazi wafunguka
Baada ya Lipumba kuzungumza, wakazi waliokuwapo ukumbini hapo walipata fursa ya kutoa dukuduku ambapo wengi wao walitaka mawaziri watatu wang’olewe madarakani.

Waziri Nchimbi anatakiwa kung’olewa kwa sababu ya kutowachukulia hatua polisi waliokwenda kutuliza ghasia mkoani humo kuendesha vitendo vya kihalifu, kubaka na kuwanyanyasa wananchi.

Mmoja wa wakazi hao alisema Nchimbi alisema damu ya polisi iliyomwagika haitapotea bure wakati askari hao walikufa kwenye ajali wakiwa njiani kwenda Mtwara.

“Polisi hawakufa kwenye mapambano, walikufa kwa ajali ya gari lao sasa wananchi watalipa vipi vifo hivyo? Waziri Nchimbi alichemka na hatufai,” alisema mkazi huyo.

Pia wananchi hao walimtaka Waziri Shamsi Vuai Nahodha aondolewe madarakani kwa kushindwa kuulinda mkoa huo pamoja na kutowawajibisha wanajeshi waliokiuka maadili ya kazi zao wakati wakilinda usalama mara baada ya kutokea kwa vurugu.

Mwananchi mwingine alitaka Waziri Muhongo aondolewe kwa kuwa ameshindwa kusimamia suala hilo la gesi lililo chini ya wizara yake na hivyo kusababisa vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top