ASKARI 15 wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
waliofukuzwa kazi hivi karibuni kwa kosa la kupokea rushwa ili kupitisha
mizigo bandarini kwa njia za magendo wameibuka na kutoa siri ya
kufukuzwa kwao.
Mmoja wa askari hao akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema sababu
ya kufukuzwa kwao imetokana na wao kukamata magari ya vigogo serikalini,
akiwemo aliyekuwa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ), ambaye anadaiwa kuwa kinara wa kukwepa kodi.
Akizungumza na gazeti hili, askari huyo alisema baadhi ya viongozi wa
juu wa jeshi hilo wamekuwa wakiwasaidia wafanyabiashara wakubwa kukwepa
kodi na pindi askari wadogo wanapoyakamata magari hayo hufukuzwa kama
ilivyotokea kwao.
Kwa mujibu wa habari hizo, katika kesi ya kijeshi iliyotolewa hukumu
ya kuwaondoa kazini askari hao, waliomba waoneshwe dereva na gari
linalodaiwa kuwa lilitoa rushwa kwao kama kielelezo muhimu katika kesi
yao, lakini hadi sasa gari na dereva huyo hawajapatikana.
Mashtaka ya askari hao, yalitarajiwa kusomwa na askari mmoja wa juu,
lakini alipobaini kwamba hakuna ushahidi, aliamua kujiondoa na
kuchukuliwa na askari mwingine ambaye ndiye aliyewasomea mashitaka.
“Baada ya kesi kusomwa Juni sita mwaka huu, ikatolewa hukumu ya
kutuondoa kazini pasipo walalamikaji na vidhibiti kuwasilishwa katika
mahakama ya kijeshi. Kwa kifupi hatukutendewa haki na tunakusudia kukata
rufaa,” alisema askari huyo kwa niaba ya wenzake.
“Ukweli ni kwamba wanaofanya baiashara ya kuingiza bidhaa bila kulipia
kodi ni viongozi wakubwa wa nchi hii hasa huyu kiongozi mstaafu wa
Zanzibar na mkewe, sisi leo hatupo kazini na wao wanaendelea kupitisha
bidhaa bandarini kwa rushwa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, akizungumzia
hatua ya askari hao kufukuzwa kazi alisema alichofanya ni kuthibitisha
adhabu yao baada ya kupitishwa katika kitengo cha nidhamu ya jeshi.
“Kwangu si muhimu kujadili adhabu iliyotolewa na mahakama ya kijeshi,
nilichofanya ni kuthibitisha tu na kama wanaona wameonewa, tumewaambia
wakate rufaa,” alisema Wambura.
Akizungumzia madai ya kuwalinda baadhi ya viongozi katika tuhuma za
kusafirisha mizigo pasipo kulipia ushuru, Kamishna wa Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma
hizo aziwasilishe kwake.
Kuhusu kukosekana ushahidi pamoja na wahusika waliotumika kutoa
rushwa, CP Kova, alisema hawezi kuwataja kwa kuwa walitumwa kuweka mtego
wa kuwanasa askari wanaosaidia watu kukwepa kodi.
Taarifa za kukamatwa kwa askari hao, zilifichuliwa na gazeti hili na
kuripoti kuwapo kwa mtandao mpana wa askari wa jeshi hilo wanaojihusisha
kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi.
0 comments:
Post a Comment