Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mshariki, Samuel Sitta.

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mshariki, Samuel Sitta, ameionya Kenya kutokana na mipango yake ya siri ya kuichafua Tanzania. 

Sitta alisema mipango hiyo ya Kenya imedhihiri baada ya gazeti la Sunday Nation kuchora katuni ambayo ililifananisha Bunge la Tanzania na klabu ya pombe. 

Sitta alisema katuni hiyo iliyotolewa hivi karibuni na gazeti hilo, ilionekana wazi kulidhalilisha Bunge la Tanzania. Alisema uhuni huo haukubaliki. Kwa mujibu wa Sitta, katuni hiyo ilichora Bunge la Tanzania wabunge wake wakiwa wamelewa chakari na wengine wakiwa nusu uchi.

Alitoa karipio hilo bungeni jana muda mfupi kabla ya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

“Hivi karibuni gazeti la Sunday Nation lilichora katuni chafu ikionyesha Bunge la Tanzania sawa na klabu ya pombe.

“Huu ni udhalilishaji, ukiangalia katuni hiyo wabunge wetu wanaonekana wamelewa, wengine wamezungukwa na chupa, wengine wamevaa nguo za ovyo ovyo.

“Huu ni uhuni haukubaliki, tunalaani jitihada zozote zinazofanywa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za kuichafua Tanzania, ” alisema.

Sitta alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo zinaendelea kutekeleza hatua mbalimbali kuelekea katika Shirikisho la Siasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hatua hizo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja (Common Market), Umoja wa Fedha (Sarafu Moja) na baadaye Shirikisho la Siasa.

Kuhusu sarafu moja, Sitta alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo zipo katika hatua ya mwisho kujadiliana kupitisha rasimu ya mpango kazi kuelekea katika hatua hiyo.

Kwa mujibu wa mpango huo, masuala ya msingi yatakamilika baada ya kukamilika kwa itifaki itakayotiwa saini Novemba mwaka huu.

Gharama za uanachama zaongezeka
Sitta alisema mchango wa Tanzania katika jumuiya hiyo umeongezeka kutoka Sh bilioni 8.8 mwaka jana hadi Sh bilioni 12.4 mwaka huu ambalo ni ongezeko la asilimia 17.

“Tofauti hiyo ya ongezeko la michango ya jumuiya na bajeti ya wizara inaonyesha kuwa gharama za uanachama wetu katika jumuiya zimeongezeka bila kuzingatia ipasavyo mipango ya kunufaika na uanachama wetu katika jumuiya hiyo,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top