Sir Alex Ferguson
Uongozi wa Old Trafford umetangaza rasmi na
kuthibitisha kuwa David Moyes atakuwa meneja mpya wa timu hiyo kuchukua nafasi
ya Sir Alex Ferguson atakayestaafu mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Old
Trafford mchana wa leo, David Moyes amepewa mkataba wa miaka sita wa
kuifundisha Manchester United kuanzia msimu ujao.
David Moyes mwenye umri wa miaka
50,ametangazwa kuwa mrithi wa Ferguson ambaye alitangaza kustaafu kuifundisha
Manchester United mwishoni mwa msimu huu baada ya kuifundisha United kwa karibu
miaka 27.
"Tumekubaliana kwa pamoja bila
kipingamizi kupitisha jina la David Moyes" alisema Ferguson.
"David ni mtu ambaye ana
uadilifu wa hali ya juu na mwenye maadili makubwa ya kazi. Nimeipenda kazi yake
kwa muda mrefu tangu mwaka 1998 wakati tulipomjadili kama kocha msaidizi.
"Hakuna maswali juu yake na ana
viwango ambavyo tulikuwa tunavihitaji kwa meneja wa klabu hii." aliongeza
Ferguson.
Naye David Moyes amesema "
Najua ni vigumu kurithi na kufikia mafanikio kama ya kocha bora zaidi duniani,
lakini nafasi ya kuifundisha Manchester United sio jambo ambalo linakuja mara
mbili hivyo nina matumani mazuri nikiwa kocha wa klabu hii msimu ujao."
David Moyes amekaa Goodison Park kwa
miaka 11 na hajawahi kushinda taji la ligi kuu lakini ameweza kuifanya Everton
kuwa miongoni mwa klabu zenye mafanikio ya wastani kwenye ligi kuu soka nchini
England.
Akiwa na Everton, Moyes ameifikisha
fainali ya kombe la FA mwaka 2009 katika mechi waliyofungwa na Chelsea 2-1, na
pia mwaka 2005 aliweza kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu ya
England lakini waliondolewa kwenye hatua za mwanzo za kusaka nafasi ya
kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.
Licha ya kuwa na bajeti ndogo ya
usajili, Moyes aliiwezesha Everton kuonekana miongoni mwa timu zenye kiwango
bora cha soka ambapo mara kadhaa amekuwa akitoa upinzani mkubwa kwa Manchester
United ambapo katika mechi ya kwanza ya ligi kuu msimu huu, Everton waliifunga
United kwa bao moja kwa bila.
Kibarua kikubwa ambacho anatarajia
kukikabili kama meneja mpya wa United msimu ujao itakuwa ni kuhakikisha
mchezaji wake wa zamani aliyemuibua Wayne Rooney anasalia kwenye klabu hiyo
baada ya kutangaza kuwa anataka kuondoka.
Meneja wa Wigan, Roberto Martinez na
bosi wa Swansea, Michael Laudrup wanatajwa kama warithi wa Moyes kwenye klabu
ya Everton.
Mechi ya kwanza ya David Moyes kama
kocha mpya wa Manchester United inatarajia kuwa ya ngao ya jamii watakapo
pambana na watani zao Manchester City ama Wigan hapo tarehe 11 mwezi wa nane
kwenye uwanja wa Wembley.
MAN.UNITED YASEMA ROONEY HAUZWI
Rooney akiwa na Kocha David Moyes aliyemtoa kisoka.
Klabu ya Manchester United imepuuzilia mbali uvumi
uliozagaa ya kwamba Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uingereza anayekipiga katika
timu hiyo Wayne Rooney atauzwa mwishoni mwa msimu huu.
Manchester United imekanusha uvumi huo kupitia
Msemaji wa Klabu hiyo umesema hakuna mpango wowote wa kuuzwa kwa Mshambuliaji
huyo aliyetumikia timu hiyo kwa miaka tisa sasa.
Msemaji wa Manchester United
amesisitiza Rooney mwenye umri wa miaka 27 ataendelea kuwepo katika klabu hiyo
na hawezi kuondoka eti kwa kuwa Kocha Mkuu Sir Alex Ferguson ametangaza
kustaafu mwishoni mwa msimu huu.
Tamko la Manchester United limekujwa
baada ya kuwepo taarifa Rooney ameomba kuondoka kwa mara ya pili katika kipindi
cha miaka mitatu sasa taarifa ambazo zimetajwa kuwa ni uzushi mtupu.
Taarifa hizi zinakuja na kuongezewa
nguvu ya kwamba Rooney alishamuomba Sir Ferguson kuondoka Manchester United
kipindi cha majuma mawili yaliyopita lakini ombi lililokataliwa na Kocha huyo.
Rooney anatajwa kuwa aliomba
kuondoka Manchester United na kumueleza Sir Ferguson ya kwamba huu ni wakati
wake muafaka kuondoka baada ya kuitumikia Klabu hiyo kwa kipindi cha miaka tisa
akitokea Everton.
Uvumi wa kuondoka kwa Rooney unakuja
ikiwa ni siku moja baada ya Sir Ferguson kutangaza kustaafu wadhifa wake na
wengi walianza kutoa taarifa hizo punde tu baada ya mchezaji huyo kuonekana
akikosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
Mshambuliaji huyo anaelezwa alikuwa
na hasira baada ya kuwekwa benchi katika mchezo dhidi ya Real Madrid ambapo
Danny Welbeck alianza kwenye mchezo huo ambao Manchester United haikufanya
vizuri.
Rooney msimu huu amekuwa
akibadilishwa mara kadhaa tangu Manchester United imsajili Robin Van Persie
ambaye alipewa jukumu la kuwa mshambuliaji kinara na kuweza kuisaidia kutwaa
taji la 20.
Tangu Rooney ajiunge na Manchester
United mwezi Agosti mwaka 2004 amecheza michezo 402 na kufunga magoli 197 huku
msimu huu akifunga magoli 16 katika michezo 37 aliyoshuka dimbani.
1 comments:
Moyes nadhani ana changamoto kubwa. Hii itamuwezesha kukua na hata kuwa moja ya makocha bora duniani.
Post a Comment