Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa Mulongo
VIGOGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo wabunge, wamemjia juu
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa Mulongo kwa jinsi alivyoshughulikia
kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).
Wabunge hao waliliambia gazeti hili mjini Dodoma kuwa kesi ya
uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Lema kwa shinikizo la mkuu
huyo, itaiathiri kwa kiasi kikubwa CCM.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema kuwa amefuatilia kwa makini
chanzo cha kesi ya Lema na hatimaye kukamatwa na polisi mithili ya
gaidi, na kubaini kuwa hulka za utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa
serikali zinawapa sifa na umaarufu zaidi CHADEMA.
“Mimi sitaki kuingilia kesi, lakini ukiangalia kuanzia ile inayoitwa
video ya vurugu za Chuo cha Uhasibu Arusha na jinsi Mkuu wa Mkoa
alivyofika eneo la tukio na kuondoka, utabaini udhaifu mkubwa wa
kiongozi huyo ambao leo unamfanya Lema aonekane shujaa.
“Leo tunaingia kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani pale Arusha, tunaweza
tukashinda, lakini tutafanya kazi ya ziada kwa sababu tu ya udhaifu wa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha,” alisema Lugola.
Mbunge mwingine ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema
alichokifanya Mulongo ni sehemu ya tatizo kubwa la viongozi wa serikali
kujihusisha na ukereketwa wa kisiasa.
“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa kuna kiongozi, tena
hakumtaja jina, kwamba anapendwa kubebwa, alisema mwacheni abebwe.
Alisema vile kuwazuia polisi kukabiliana na watu wanaopenda kumbeba
kiongozi huyo.
“Mkuu wa Mkoa Arusha na wengine wanaokabiliana na wapinzani kwa nguvu
kubwa bila sababu, hii inawaongezea umaarufu,” alisema mbunge huyo
kutoka moja ya majimbo ya kanda ya kati.
Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya CCM ambaye pia hakutaka kutaja jina
lake, alilaani jinsi mkuu wa mkoa huyo alivyojikoroga katika
kushughulikia mzozo wa Chuo cha Uhasibu Arusha.
“Niliposoma ujumbe wa simu ya mkononi wa Lema ambao alidai umetoka kwa
Mkuu wa Mkoa, nilishangaa sana. Sijui kwa nini amefanya vile,” alisema
kigogo huyo.
Aprili 24 mwaka huu, Mulongo aliliamuru Jeshi la Polisi mkoani Arusha
kumkamata Lema kwa madai kuwa aliwachochea wanafunzi wa chuo hicho cha
IAA kumzomea na kumrushia mawe.
Lema alizingirwa nyumbani kwake na maofisa wa polisi kitengo cha
upelelezi na wale wa doria Ijumaa saa 5.30 usiku kisha kuchukuliwa hadi
Kituo Kikuu cha Polisi kuhojiwa na kuwekwa rumande siku tatu hadi
Jumatatu wiki hii alipofikishwa mahakamani.
Hata hivyo, madai ya Mulongo kuwa Lema alichochea wanafuzni hao
yanakinzana na ushahidi wa video unaoonesha kuwa mbunge huyo alitumia
kila aina ya ushawishi kuwasihi wasiandamane kufuatia mwenzao Elly Kago
(22) kuuawa na watu wasiojulikana jirani na chuo.
Mapema kabla ya kukamatwa, Lema aliitisha mkutano na waandishi wa
habari akidai kutishiwa na Mulongo kupitia ujumbe wa maandishi wa simu.
“Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni
serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’
ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba 0752 960276 ambayo
Lema alidai ni ya Mulungo.
Atisha waandishi
Wakati CCM wakiendelea kumlalamikia Mulongo kwa hatua zake dhidi ya
Lema, kiongozi huyo jana aliwageukia waandishi wa habari wa Arusha
akiwataka wawe makini kipindi hiki, akidai kuwa nao wanatumika na
wanasiasa.
Akihutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi, alisema kuwa
ikibainika wanatumika nao watafikishwa katika vyombo vya sheria.
“Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya Bagamoyo, hivi hivi wakawa hawanielewi
na ikafika wakati wakanielewa kwani kuna miongoni mwao tulitaka
kuwafikisha katika sheria, lakini tukayaacha kwa kuwa sisi ndio walezi,”
alisema.
Mulongo aliongeza kuwa vitu ambavyo vinaandikwa si kweli kabisa, na
kwamba wataendelea kufuatilia kwani baadhi ya waandishi wanashirikiana
na wanasiasa kuwachafua viongozi wa serikali.
Alisema baadhi ya waandishi mkoani Arusha wamekuwa wakifanya kazi zao
kwa ushabiki wa kisiasa na kuandika mambo ambayo hawana uhakika nayo.
“Unapoingia katika mkakati wa kudhalilisha kiongozi wa serikali unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni makini,” alisema.
Aidha alivionya vyama vya wafanyakazi mkoani Arusha kutoruhusu
kutumiwa na watu kwa malengo ya kisiasa na pia waajiri waache kufanya
kazi bila kufuata taratibu na sheria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment