Waziri Mkuu Mizengo Pinda
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema utaratibu wa elektroni uitwao biometric ambao umeanza kuandaliawa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), utasaidia kuondoa malalamiko ya wizi wa kura.

Pinda aliyasema hayo jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Hai ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema).

Kwa mujibu wa Mbowe utaratibu huo ulijaribiwa Ghana na Kenya na ukawaletea matatizo.

Kutokana na hali hiyo, alitaka kujua kama Pinda yuko tayari kusimamisha mfumo huo ili wadau mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa vitakaposhirikishwa.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema swali alilouliza Mbowe ni mwendelezo wa hofu iliyojengeka katika mifumo ya uchaguzi na kwamba imekuwa hofu zaidi hata kura zinapohesabiwa kwa mkono.

“Utaratibu huo unaweza kutupa matunda mazuri kwani unaweza kutuondolea matatizo kwa kiasi kikubwa.

“Sasa mimi sina details za jinsi walivyojiandaa na mfumo huo ingawa jitihada hizi za tume zina nia nzuri kwani utaratibu huo asilimia 100 ni wa kitalaamu na ni lazima wadau washirikishwe,” alisema.

Aliwataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuiamini NEC kwa kuwa ina watu makini ambao haamini kama wanaweza kusababisha makosa yasiyofaa.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top