MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy Mohammed.
 
 MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy Mohammed (CCM) ameishauri Serikali kuachana na kuhamasisha kilimo cha tumbaku kwa vile kinasababisha magonjwa ya kansa; badala yake iruhusu kilimo cha bangi.
 
Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, Kessy alisema zao la tumbaku linapingwa kote duniani; hivyo sio vyema kwa Serikali kuendelea kuhamasisha kilimo chake na ni vyema ikaruhusu bangi kwa vile ina uwezo wa kuliletea taifa fedha za kigeni.
 
“Kwa nini tusiruhusu kilimo cha bangi kuliletea taifa fedha za kigeni badala ya kuhamasisha kilimo cha tumbaku?” Alihoji mbunge huyo na kusababisha wabunge kulipuka kwa kicheko.
 
Katika majibu ya Serikali, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alisema ni kweli kwamba zao la bangi limesharuhusiwa katika baadhi ya nchi hapa duniani.
 
Lakini alisema kwa hapa nchini hawawezi kuruhusu kilimo cha zao hilo kwa sababu bangi bado inachukuliwa kama ni zao la dawa za kulevya na linapingwa katika baadhi ya nchi.
 
“Siku tukijiridhisha kuwa bangi imepata uhalali duniani kote na imekubaliwa kulimwa na sisi tutaelekea kwenye kilimo cha zao hilo lakini kwa sasa hatukiruhusu,” alisema Malima.
 
Alisema katika kipindi hiki sio wakati wa kupuuza kilimo cha tumbaku kwa vile ndilo zao pekee ambalo kwa sasa linalipatia taifa fedha nyingi za kigeni.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top