Makazi ya mkazi wa kitongoji cha Bwila Chini kijiji cha Bwila Chini kata ya Selembala akiwa amesimama nje ya nyumba yako kukumbwa na mafuriko katika kata hiyo ambapo jumla ya kata nne za wilaya ya Morogoro Vijijini kukumbwa na mafuriko April 5 mwaka huu mkoani Morogoro.  

 Wakazi wa kijiji hicho wakiwa nje ya nyumba yao wakati wanamsubiri mbunge wao wa jimbo hilo la Morogoro Kusini,Innocent Kalogeris.
Mbunge wa Morogoro Vijijini, Innocent Kalogerisakizungumza na mkazi wa Bwila Chini baada ya nyumba yake kubomoka baada ya kukumbwa na mafuriko.
 Mkazi wa kijiji hicho cha Bwila Amina Omari akiwa nje ya nyumba yao juu baada ya kukumbwa na mafuriko.
 Wakazi wa kijiji cha Bwila Chini wakitembea kwenye maji baada ya maji hayo kutuwama katika barabara na mashamba yenye mimea ya mahindi.
 Muonekano wa nyumba iliyokumbwa na mafuriko hayo.
 Mmea wa mhindi ukiwa umeng'olewa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha April 5 mwaka huu.
 Mimea ya mahindi ikiwa imelala chini baada ya mvua kunyesha iliyoambanata na upepo katika kijiji cha Dutumi.
 Sehemu ya wakazi wa Bwila Chini wakiwa eneo la nyumba yao ambayo ilibomoka kutokana na mafuriko hayo.
 Watoto wa kijiji cha Bwila Juu akiwa wamebeba kiroba cha unga baada ya mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris kutoa msaada wa kilo 450 za unga wa mahindi kwa ajili ya kuwagawia wazee wasiojiweza katika kata ya Selembala.
 Wakazi wa Bwila Chini wakiwa nje ya nyumba yao ambayo imezingirwa na maji.
 Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris akitembea kwenye maji wakati akielekea katika kijiji cha Bwila Chini kugawa unga kwa wazee wasiojiweza wanaoishi katika kata ya Salambala.
ZAIDI ya kaya 450 katika kata nne tofauti zimekumbwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa kunyesha ambapo imebomoa nyumba, kusomba mifugo ikiwemo na kuharibu heka 233 za mimea ya mazao aina mbalimbali baada ya mvua kubwa kunyesha April 5 mwaka huu katika wilaya ya Morogoro Vijijini.
Akizungumza na wananchi wakati wa ugawaji wa chakula kwa wazee wasiojiweza kata ya Selembala Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris alisema kuwa mpaka sasa kuna kata nne ambazo zimekumbwa na mafuriko ambapo kaya zaidi ya 450 zimeathirika kutokana na mafuriko hayo.
Kalogeris alisema kuwa kutokana na mvua hiyo kunyesha na kusababisha mafuriko kaya hayo wananchi wamepoteza mali mbalimbali ikiwemo chakula, mifugo na kuharibu mimea ya mazao aina mbalimbali katika kata hizo.
“Njia ya kuwanusuru wananchi hao ambao wamekumbwa na janga la mafuriko kwa sasa kunahitajika zaidi ya tani 70 ama 80 za chakula cha haraka kwa ajili ya kuwagawia wahanga hao ili kuwanusuru na janga la njaa pamoja na kupatiwa mbegu za muda mfupi ili kuweza kupanda katika mashamba yao”. Alisema Klaogeris.
Kalogeris alisema kuwa kwa upande wa mbegu za muda mfupi zinahitajika  tani 50 hadi 60 kwa ajili ya kupanda katika kipindi hiki cha mvua za mwisho ili kuweza kupata mavuno yatayosaidia katika msimu ujao wa kilimo.
Alitaja kata zilizokumbwa na mafuriko hayo kuwa ni pamoja na Kisaki,  Bwakila Chini, Mvuha Selembala huku wananchi wa kata ya Selembala wakiathirika zaidi na mafuriko hayo.
Alisema kuwa leo (jana) nimetoa taarifa katika kamati ya ulinzi na usalama juu ya uhitaji wa tani za chakula na mbegu kwa waathrika hao.
Kalogeris aliongeza kuwa tayari mkuu wa wilaya ya Morogoro Saidi Amanzi ametoa maagizo kwa maafisa watendaji wa vijiji kufanya tathimini ya kiwango cha uharibifu wa mali na mimea ili kuweza kupata idadi kamili ya uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo.
Katika mafuriko hayo kata ambayo imeathirika zaidi ni kata ya Selembala ambapo jumla ya nyumba 77 zimeharibika na heka za mimea ya mahindi, uvuta 233 katika kitongoji cha Bwila Chini.
Mbunge huyo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Morogoro alikabidhi unga kilo 450 katika vitongoji vitano kwa ajili ya wazee wasiojiweza 30 wa kijiji cha Bwila Juu kupitia kwa vitongoji vya Kibiro, Umoja, Songambele na Muhunzi ambao kila kitongoji wazee sita walipatiwa unga katika kata hiyo.
Mafuriko hayo yalitokea baada ya mvua kubwa kunyesha kwa masaa 24 ikianza majira ya saa 4 usiku April 5 mwaka huu na kuharibu mali mbalimbali ikiwemo nyumba, mifugo, mimea ya mazao na kupelekea baadhi ya wahanga wa mafuriko hayo kushinda juu ya miti kwa muda wa masaa matatu.
via Juma Tanda
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top