KAULI ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Stephen Wassira kudai kuwa Idara ya Usalama wa Taifa haiwezi kumtesa
Kibanda kwa kuwa hana umaarufu kisiasa nchini, imeibua mjadala mkali,
Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Juzi wakati akihitimisha hoja ya hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa
mwaka wa fedha 2013/ 2014, Wassira aliitetea Idara ya Usalama wa Taifa
dhidi ya tuhuma zinazowahusu baadhi ya watendaji wake kuhusika katika
matukio kadhaa ya utekeji na utesaji wa raia.
Wassira alisema haiwezekani kwa watumishi wa idara hiyo kujihusisha na
matukio hayo na kueleza mafanikio mbalimbali ambayo imeliletea taifa.
Alihoji sababu za kulihusisha tukio la kutekwa na kuteswa kwa
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda na idara
hiyo na kuhoji; ‘kwani yeye ni nani?’
Katika kuali hiyo ambayo imeibua mjadala, Wassira alisema haiwezekani
idara hiyo ikahusika kwa kuwa Kibanda hana umaarufu katika siasa za
Tanzania, na kwamba labda wangekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod
Slaa angeelewa.
Kibanda alivamiwa akiingia nyumbani kwake Mbezi Juu jijini Dar es
Salaam usiku wa Machi 6 mwaka huu na watu wasiojulikana, na kushambuliwa
vibaya kwa kupigwa nondo kichwani, kutobolewa jicho la kushoto,
kung’olewa ukucha, meno mawili na kukatwa kidole.
Kauli ya Wassira imepokelewa kwa mtazamo hasi na watu mbalimbali
katika jamii, huku wengi wakisema kuwa hiyo ni ishara kwamba chombo
hicho kinahusika na vitendo hivyo, lakini kwa kundi fulani la watu.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, mwanasheria maarufu nchini,
Mabere Marando alisema mjadala huo unatokana na hoja aliyoanzisha yeye
ya kuwataja watu wa Usalama wa Taifa kuwa wanahusishwa na utekaji na
utesaji.
Marando ambaye pia ni ofisa wa zamani wa idara hiyo, alifafanua kuwa
ni vema Wassira ashauri sera za Idara ya Usalama zifanyiwe mabadiliko,
waache kulinda heshima ya chama badala yake walinde taifa.
“Kazi za usalama ni kugundua mapema na kutoa taarifa habari zinazohusu
serikali kupinduliwa, kusaidia serikali katika ujasusi wa uchumi ili
nchi iendelee na mwisho kabisa ni kushauri serikali kuhusu hali ya
kisiasa nchini. Wala sio kupambana na wanasiasa au waandishi wa habari,”
alisema.
Marando aliongeza kuwa Usalama wa Taifa sasa unafanya kazi za usalama
wa raia ambazo ni za polisi kimsingi. Kwamba Usalama wa Taifa huwa
hawakamati, lakini siku hizi wanakamata.
“Sasa kama hawa wakifanya hivi polisi watafanya kazi gani? Tunashindwa
kutofautisha kazi za usalama wa taifa na usalama wa raia,” alisema.
Katibu wa TEF, Neville Meena alisema kuwa Wassira ni kielelezo cha
ulevi wa madaraka. Anaona kuwa wanasiasa ndio watu zaidi kuliko wengine.
Alisema kwa kauli ile pengine ndiyo maana uchunguzi wa suala la
Kibanda haufanyiki wala hakuna taarifa rasmi ya polisi iliyotolewa tangu
atekwe na kuteswa.
“Tunafurahi kwa kuwa tumepata mawazo ya watawala na kauli ya Waziri
huyu wa Nchi, Ofisi ya Rais pengine ndiyo msimamo wa serikali maana
alisema bungeni.
“Huyu anatoka Ofisi ya Rais, tena anashughulikia mahusiano. Anapotoa
kauli hii zikiwa zimefika siku 45 tangu Kibanda atekwe na kuteswa,
mauaji au mateso kama hayo hayataisha katika nchi kwa kuwa sisi wengine
sio watu kwa mujibu wa Wassira. Kauli hii ni mbaya na haina afya,”
alisema Meena.
Mwandishi nguli wa habari nchini na mshauri wa masuala ya habari,
Ndimara Tegambwage alisema; “Kwanza tunafurahi kwa kuwa Wassira
amethibitisha kuwa wana usalama wanawaandama watu na mara zingine
kuwadhuru viongozi wakubwa hasa wasiofuata au kukubaliana na sera zao.
“Pili, kwa mujibu wa Wassira kwa sasa Watanzania tunajua kuwa baya
lolote likimpata Dk. Slaa au Mbowe litakuwa limetekelezwa na watu wa
usalama.”
Ndimara aliongeza kuwa kwa kauli ya Wassira kusema kuwa Idara ya
Usalama inashughulikia wanasiasa maarufu, ameivua nguo idara hiyo na
wangetarajia idara hiyo imwajibishe kwa kutoa siri za Usalama wa Taifa.
“Linapokuja suala la haki za binadamu hakuna mdogo au mkubwa, hakuna
rais au mama ntilie. Hakuna aliye mdogo asiyehusiana na mkubwa, ikifikia
hatua ya dharau ya aina hii tunashindwa kumwelewa waziri huyu,”
alisema.
Mkurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za
binadamu, Onesmo Olengurumwa alisema Wassira amethibitisha kuwa kumbe
Usalama wa Taifa kuna watu wanawateka na kuna wengine hawatekwi.
“Tunashukuru kwa kusema kuwa kuna kundi fulani linawindwa, ni dharau
sana kwa kauli ile kwa kuwa Kibanda ni Mtanzania, awe na cheo asiwe na
cheo, awe mwanasiasa au sio mwanasiasa serikali inapaswa kumlinda.
“Kauli ya Wassira inaleta matabaka, inaonesha wengine wana thamani zaidi, wengine hawana thamani,” aliema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alizungumza
kwa kifupi akisema; “hiyo kauli haikupimwa, sio kauli iliyotarajiwa
kutoka kwa kiongozi wa CCM. Kweli hakutumia busara katika kutamka kauli
hii tena bungeni.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment