KATIKA kuadhimisha miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, Rais Jakaya Kikwete kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya
ibara ya 45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ametoa msamaha kwa wafungwa
4180.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jijini
Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi,
alisema kuwa wafungwa watakaofaidika na msamaha huo ni waliokuwa
wanatumikia kifungo kisichozidi miaka mitano na kwamba watakuwa
wameshatumikia robo ya vifungo vyao.
Watakaonufaika wengine ni wale ambao walihukumiwa kifungo
kinachozidi miaka mitano ambao wamepunguziwa moja ya sita ya vifungo
vyao zaidi ya punguzo la kawaida, wagonjwa wenye magonjwa kama ukimwi,
kifua kikuu na kansa.
Wamo pia wafungwa wazee wenye miaka 70 au zaidi, wafungwa wa kike
walioingia na mimba gerezani pamoja na wale walioingia na watoto
wanaonyonya na wasionyonya.
Dk. Nchimbi alibainisha kuwa wanufaika wengine ni wale wenye ulemavu
wa mwili na akili na ambao walihukumiwa na kuwepo gerezani kwa ridhaa
ya Rais Kikwete.
Aidha, alieleza kuwa msamaha huo hautahusisha wafungwa waliohukumiwa
kunyongwa, wanaotumikia kifungo cha maisha, wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya kujihusisha na biashasra ya madawa ya kulevya, kupokea au
kutoa rushwa.
Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na
unyang’anyi wa kutumia silaha, kupatikana na silaha au risasi, kunajisi,
kubaka na kulawiti, waliopatikana na hatia ya kuwapa mimba wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari ambao walitenda makosa hayo wakiwa na
miaka 18 na zaidi.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana aliwaongoza maelfu ya Watanzania
katika sherehe hizo za Muungano, zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa
Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Rais baada ya kuwasili uwanjani alipigiwa mizinga 21 na kisha
kukagua gwaride na kupokea heshima ya majeshi ya ulinzi na usalama
yaliyopita mbele yake kwa mwendo wa pole na kasi.
Kisha zilifuata buradani mbalimbali kama vile halaiki ya watoto
2695, ngoma za asili na maonesho ya vikosi vya ulinzi ambavyo vilirusha
ndege za kivita na mafunzo hewani.
Akizungumzia Muungano huo, mmoja wa wanazuoni Profesa Mwesiga
Beregu, alisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia kwani ni wa
pekee katika bara la Afrika.
Prof. Beregu alipinga dhana ya baadhi ya watu kuwa muungano hautakiwi akisema kuwa wenye mawazo hayo si wengi.
“Wakati wa mchakato wa Katiba tulipopita Zanzibar kwa kweli
sijakutana na watu kama hao, kama wapo wanaotaka kuuvunja Muungano basi
watakuwa ni wachache,” alisema Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Naye mwananchi, Edna Sitta, alisema Muungano huu unawanufaisha zaidi
Wazanzibari ambao wana uwezo wa kujipatia hata ardhi Tanzania Bara
bila vikwazo wakati hali hiyo ni tofauti kwa wabara kumiliki ardhi
Zanzibar.
Tatu Ali (86) mkazi wa Temeke, alisema Muungano huu hauna matatizo
bali watu wanatakiwa kuwa na uvumilivu pia na kujiepusha kupenda makubwa
ambayo mara kadhaa yamekuwa yakijenga taama.
Viongozi mbalimbali walihudhuria sherehe hizo wakiwemo marais
wastaafu, Alhaji Alli Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Amani Abeid Karume,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mawaziri wakuu wastaafu na wengineo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment