Latest News

 Na James Gashumba , EANA
 Bunge la Afrika Mashariki (EALA) siku ya Alhamisi lilipitisha sheria ya kuanzishwa kwa Kituo Kimoja cha Forodha Mipakani (OSBP) katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Azimio hilo lililoibuliwa na Baraza la Mawaziri la EAC ni moja ya agenda za kukuza mwingiliano wa watu na biashara katika Jumuiya hiyo ambapo nchi wanachama ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.


Sheria hiyo itaweza kutumika katika uendeshaji wa vituo vya forodha vya mipakani,uratibu na usimamizi wake.


Hata hivyo sheria hiyo haitaathiri haki ya nchi mwanachama ya kufanya uchunguzi kwa minajili ya ulinzi, usalama, usalama wa umma na utii wa sheria.
 
Sheria hiyo pia imeorodhesha vituo vilivyo katika utaratibu huo wa
OSBP. Vituo hivyo vya mipakani ni pamoja na Taveta-Holili na Namanga (Kenya-Tanzania), Busia na Malaba (Kenya –Uganda) na
Kanyaru-Akanyaru(Burundi- Rwanda). Vingine ni Mutukula
(Tanzania-Uganda),Gasenyi-Nemba (Burundi-Rwanda) na
 
Lungalunga-Horohoro (Kenya-Tanzania).
Mjadala juu ya sheria hii ulitanguliwa na uwasilishwaji wa ripoti ya
Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (CTI) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Dan Kadega kutoka Uganda.


Sheria hiyo inataka nchi wanachama kuendeleza, kuboresha, kuweka miundombinu ya kisasa na kuimarisha teknolojia ili kuhakikisha kuwepo kwa ufanisi katika utekelezaji wa sheria hii.


Iliwasilishwa baada ya mjadala ulifanyika katika nchi wanachama Machi na Aprili, mwaka huu ili kupata maoni kutoka kwa wadau wakiwemo maafisa wa forodha, mawakala wa mizigo na jamii ya wafanyabiashara.

Utaratibu wa OSBP umekuwa ukitumika katika baadhi ya vituo vya forodha vya mipakani kwa makubaliano baina ya nchi na nchi lakini ilibainika kwamba sheria juu ya utaratibu muafaka utakaotumika katika nchi zote wanachama unahitajika, kwa mujibu wa ripoti ya kamati
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top