David Kafulila
LICHA ya kuwepo kwa kesi ya kupinga kuenguliwa uanachama katika
Mahakama Kuu ya Tanzania, Chama cha NCCR-Mageuzi, kimesema kuwa kiko
kwenye hatua ya mwisho ya kumrejesha kundini mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila.
Kafulila na wenzake sita akiwemo aliyekuwa mgombea urais mwaka 2010,
Hashim Rungwe, walifukuzwa uanachama Desemba mwaka 2011, wakidaiwa
kukihujumu chama na kutaka kumpindua mwenyekiti, James Mbatia.
Hata hivyo, baada ya NCCR-Mageuzi kuwasilisha barua kwa Spika wa Bunge
ili kumtaarifu kuwa Kafulila si mwanachama wao tena, mbunge huyo na
wenzake walifungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo wa chama; kesi
hiyo inaendelea hadi leo.
Uamuzi huo wa kumsamehe Kafulila ulitangazwa juzi mkoani Kigoma na
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza, wakati akihutubia mkutano wa
hadhara kata ya Nguruka.
Ruhuza aliwaambia wakazi hao kuwa ugomvi kati wa mbunge wao Kafulila
na mwenyekiti wa chama, Mbatia, hivi sasa umekwisha kabisa.
“Nataka niwahakikishie wanachama wenzangu kuwa ‘kale kamgogoro
mlikokuwa mnakasikia kati ya mwenyekiti na mbunge wenu hivi sasa
kamekwisha’ kabisa, hivi sasa wanafanya kazi kwa kushirikiana kujenga
chama,” alisema.
Ruhuza alisema Kafulila alikaa na kutafakari na kugundua kuwa alichokuwa anakifanya si sahihi na hivyo kuamua kuomba radhi.
Alisema kuwa kabla ya kusamehewa alipewa mashariti ya kutimiza vigezo
fulani ili msamaha wake uweze kukubaliwa na mpaka sasa tayari mashariti
yote ameyakamilisha kwa mujibu wa katiba na taratibu za chama.
Katibu huyo aliongeza kuwa Halmashauri Kuu ya chama hicho ilikaa kikao
chake Septemba mwaka jana na kupokea ombi la msamaha wa Kafulila na
kulikubali.
“Halmashauri Kuu itakaa tena kikao mwezi ujao tarehe sita na Kafulila
atasamehewa rasmi na kuifuta kesi yake. Nataka niwahikikishie wakazi wa
Nguruka mbunge wenu ni mtu safi na mchapakazi mzuri, yale matatizo
yaliyotokea naamini ni shetani tu alimpitia na hivi sasa yuko sawa,”
alidai Ruhuza.
Kafulila ambaye kwa sasa anahesabika kama mbunge wa mahakama, ili
aweze kurejeshewa uanachama wake, inatakiwa yaandaliwe makubaliano kati
ya chama na wale waliofungua kesi kisha yasajiliwe mahakamani ili kesi
ifutwe na chama kifute uamuzi wake wa kuwafukuza.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment