29/03/2013

Kumb Na. JJM/2013/ELIMU/19

Kwa Mwenyekiti

Tume ya Elimu  ya Kufeli KIV

Ofisi ya Waziri Mkuu

DAR ES SALAAM

Ndugu Mwenyekiti

KUONGEZEKA WANAOFELI KIV KUTOKA 9.7% MWKA 2007 HADI 60% 2012

1.1   Ninawapongeza kwa kuteuliwa na ahsante kutupa fursa wadau wa elimu kuwaletea maoni na  au/ushauri.
2.0  Mimi ni mdau wa elimu, niliyewahi kuwa Mwenyekiti mwanzilishi wa Mufindi Education Trust (MET) iliyoanzisha katika wilaya ya Mufindi        na kuziendesha  kwa mika      zaidi    ya 10 Sekondari  9 za: (1) JJ Mungai (2) Sadani ( 3) Itengule  ( 4) Igowole ( 5) Itandula ( 6) Mgololo ( 7 ) Kibengu ( 8) Mdabulo na ( 9) Nyololo; ambazo sasa ni za serikali. Aidha nimewahi kuwa waziri wa Elimu na Utamaduni  mwaka 2000 hadi 2005.
3.0 Kabla ya kutoa ushauri naomba kuipa Tume yako ufahamu  wa ukweli ufuatao:
3.1 Kufeli mwaka 2012 kidato cha Nne (KIV) kwa asilimia 60 halikuwa tukio lililoibuka ghafla bali waliofeli (Division 0) mtihani huo waliongezeka kutoka mwaka 2007:9.7% ; 2008:16.3%; 2009:27.5%; 2010:49.6%; 2011:46.4% na sasa 2012:60%!!!!!
3.2 Kabla ya hapo waliofeli kidato cha Nne (KIV) WALIPUNGUA kutoka mwaka 1998:24:3%:; 1999:20.0% 2000:21.6% 2001:22.6%, 2002:12.7%; 2003:12.2%, 2004:8.7%, 2005:10.7%, 2006:10.9%, na 2007:9.7% wastani wa kufeli 2004 hadi 2007 ni 10%. Tazama hotuba ya bajeti ya Waziri wa Elimu na Utamaduni ya mwaka 2005/2006 kielelezo Na. 75.4 ukurasa wa 100; na BEST (Basic Statics in Education, National Data) ya miaka  husika.
3.3 Kati ya 2004 na 2007 waliofeli kidato cha Nne  walikuwa wastani wa 10% ambayo   inavumilika. Kwa nini kati ya 2007 na 2008 kulikuwa na mruko kutoka 9.7% hadi 16.3%? Huo ukawa ndio mwanzo wa kuongezeka  kila    mwaka    hadi kufikia 60%  ya mwaka huu!!!!! Wizara ya Elimu na OWM-TAMISEMI baada   ya  matokeo mabaya ya mwaka 2010 walifanya  “utafiti kudadisi sababu   za ufaulu huo mbaya” na taarifa yake ipo kwenye maktaba ya Wizara” na iliandaliwa kauli ya waziri isomwe Bungeni”, lakini  hadi leo haikusomwa.   Ukweli ulifichwa; na mficha ugonjwa kifo kitamuumbua. Nukuu zangu kutoka Taarifa moja     isiyo   ya siri ya ndani    ya wizara ya Elimu.
4.0 Kwa maoni yangu maboresho ya Elimu ya Serikali ya Awamu ya Tatu ambayo  yanaweza kusomwa katika maandiko   mawili    ya Wizara   ya Elimu     yaitwayo: (a) Nyaraka za Elimu 1999 hadi 2005, na ( b) Sheria ndogo za Elimu au kanuni za Elimu zilizotungwa kuyapa maboresho hayo uzito wa kisheria yamepelekwa NYARAKA ZA KALE (ACHIVES) kabla  ya wakati wake. Maboresho yamewekwa kando moja baada ya jingine  au  hayakusimamiwa ipasavyo na Elimu yetu imerudi  ilivyokuwa kabla  ya mwaka 2000.
USHAURI:
5.0 Kwa kuwa Elimu ni nyenzo muhimu   sana kuliko zote katika kuboresha nguvu kazi ya Taifa na kuchochea  maendeleo  ya nchi nimeamua kutonyamaza na kuwa muwazi kabisa, ingawaje mimi ni mwanasiasa  niliyestaafu. Kwa hiyo NASHAURI mambo yafuatayo:
5.1 Utaratibu  sahihi wa kupanda madarasa kwa ufaulu (achievement based progression)  uliowekwa na waraka wa Elimu Na. 1& 2 wa 2002 urejeshwe na uimarishwe   bila  kuchelewa kuanzia Darasa la kwanza,  la pili na la Tatu ambayo      Mwalimu Mkuu siku zote anayo madaraka ya kukalilisha, kama mwanafunzi   hajazijua “K” 3: kusoma, kuandika na kuhesabu.
5.2 Tume ya Mhe. Waziri Mkuu ifanye kwanza REJEA ya maandiko ya Wizara ya Elimu  niliyoyataja akatika 4(a) na (b) hapo  juu yaliyomo maboresho ya         elimu ya 2002-2005 yaliyofanikisha kufaulu vizuri  katika   Elimu ya Msingi na Sekondari miaka ya 2004-2007; badala ya kutumia muda mwingi na fedha nyingi kugundua upya gurudumu.
5.3 Taasisi  ya Elimu   Tanzania ( Tanzania  Institute of   Education –TIE) iagizwe na iachiwe  kutekeleza wajibu  wake wa kisheria chini ya Sheria ya Elimu ya 1995 wa kuandaa na kuboresha mitala.
5.4 Wanasiasa tuache kuamua bila  kuzingatia ipasavyo utafiti na ushauri w kitaaluma kuhusu Elimu ya Taifa letu.

Kutokana  na uamuzi mbaya na kuchelewa kuchukua  hatua ya marekebisho kila inapobidi; Elimu yetu imerudi ilikokuwa  kabla ya mwaka 2000. Rika zima la kielimu limepotea!!!sasa tunavuna kilichopandwa vibaya. Kwa hiyo TUJISAHIHISHE kwa kuacha kuingilia na kuamua bila kuzingatia  utafiti na ushauri wa kitaaluma ili tusije kuumbuliwa tena na matokeo mabaya kama  hayo ya kidato cha Nne   ya mwaka 2012. Aidha inafaa matokeo ya mitihani    yawe yanatangazwa kwa uwazi hata kama ni mabaya kwa sababu, narudia “ anayeficha maradhi kifo kitamuumbua”

Wasalamu

Joseph J Mungai MB mstf

MDAU WA ELIMU
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top