Na Joachim Mushi
UCHUNGUZI juu ya chanzo cha kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa likijengwa na kuuwa watu pamoja na kujeruhi umeanza kwa kuhusisha wataalamu wa masuala ya ujenzi wa majengo makubwa. Uchunguzi huo ambao unahusisha kuufanyia vipimo mchanganyiko wa zege lililotumika kujengea ghorofa hilo pamoja na vifaa umeanza leo mchana ikiwa ni siku moja baada ya kuanguka kwa ghorofa hilo.

Mtandao huu (Thehabari.com) umewashuhudia wataalamu wa majengo wakichukua baadhi ya mabaki ya kifusi cha jengo hilo tayari kwa kwenda kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini nini chanzo cha jengo hilo kuporomoka ghafla juzi asubuhi.

Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alishuhudia wataalamu wa majengo (wahandisi) kutoka kampuni kadhaa za ujenzi jijini Dar es Salaam waliotembelea eneo la tukio leo wakilaumu uzembe uliofanyika hadi kuporomoka kwa jengo hilo.

baadhi yao walisema kifusi kilichoporomoka kinaonesha wazi kuwa kulikuwa na uzembe kati ya uchanganyaji wa zenge, uwiano wa kokoto, mchanga na saruji pamoja na vipimo vingine jambo ambalo linaonesha huenda ndio chanzo ya kuporomoka kwa jengo hilo.

“…Ukiangalia mabaki ya kifusi hiki kama ni mtaalamu unagundua kabisa hakukuwa na ‘ratio’ (uwiano) kati ya kokoto, mchanga na saruji wakati wakichanganya zege, huu ni uzembe wa msimamizi wa shughuli nzima ya ujenzi wa ghorofa hili,” alisikika mmoja wa wataalamu hao akiwaeleza wenzake huku wakichunguza mabaki ya jengo hilo.

Baadhi ya wataalamu hao walisikika wakilalamikia ukubwa wa nondo (size) zilizotumika kwa baadhi ya maeneo wakisema ni ndogo sana ukilinganisha na zile za kawaida ambazo ndizo zilizotakiwa kufungwa katika baadhi ya maeneo ya jengo hilo. “Hapa kuna nondo za hadi milimita nane zimewekwa sehemu ambazo hutakiwa kufungwa nondo za milimita 12…,” alisema mmoja wa wahandisi hao.

Wakati huo huo idadi ya miili iliyopatikana katika kifusi kinachoendelea kuchambuliwa hadi leo jioni ni miili 21 na tayari maiti nne zimetambuliwa na kuchukuliwa na wahusika.

 Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema jumla ya maiti 19 zimefukuliwa hadi asubuhi. Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alishuhudia maiti nyingine mbili zikitolewa ikiwa ni muda mfupi tangu kauli ya Kamanda Kova kwa wanahabari hivyo kutimia 21.

Awali akifafanua zaidi Kamanda Kova alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu wanne hadi sasa ambao wanahusishwa na tukio hilo la kuporomoka kwa jengo hilo. Baadhi ya wanaoshikiliwa hadi sasa ni pamoja na Mhandisi wa Manispaa ya Ilala, Mmiliki wa ghorofa lililoanguka. Kamanda Kova amesema Polisi wamemtaka mmiliki wa Kampuni ya Lucky Construction Limited ambaye ni Diwani wa Kinondoni kujisalimisha mwenyewe pamoja na mchoraji wa jengo hilo ndani ya saa 24.

“…Hawa tunaomba wajisalimishe wenyewe ndani ya saa 24 wasisubiri tuanze kuwatafuta, tuna taarifa mmiliki wa hii kampuni ya Lucky Construction Limited ni diwani wa Kinondoni hivyo tunamtaka ajisalimishe mwenyewe maana ni mtu anayejulikana kutokana na nafasi yake kiuongozi,” alisema Kamanda Kova.

Zoezi la kusaka mili zaidi kwenye kifusi bado linaendelea kwa kushirikiana na vikosi mbalimbali vya uokoaji.

Jengo hilo la ghorofa 16 lililokuwa likiendelea na ujenzi eneo la makutano ya mtaa wa Hindilaghandi na Zanaki jijini Dar es Salaam liliporomoka ghafla jana majira ya saa mbili asubuhi na kufukia baadhi ya watu. Kwa mujibu wa taarifa za awali inasemekana kuwa kuna zaidi ya watu 60 ambao wanadaiwa kufukiwa katika jengo hilo.
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=30607 TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top