UZEMBE wa serikali kutotekeleza mapendekezo ya ripoti
iliyobaini upungufu kwenye majengo marefu ya ghorofa umeleta tena maafa
kwa watu watano kupoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa.
Tukio hilo limetokea jana asubuhi baada ya jengo la ghorofa 16
lililokuwa linaendelea kujengwa katika mitaa ya Indira Ghandi na
Morogoro kuporomoka na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa maeneo
hayo ya katikati ya jiji.
Hata hivyo, huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na watu wengine
zaidi ya 40 kuhofiwa kufunikwa na kifusi wakiwamo mafundi pamoja na
watoto waliokuwa wakicheza jirani na jengo hilo.
Jengo hilo lililoko katika kitalu Na.166 ni mali ya Raza Ndagji na mjenzi wake ni Kampuni ya Lucky Construction Limited.
Baadhi ya watu walidai jengo hilo kujengwa chini ya kiwango kutokana
na vifaa vilivyotumika, ingawa mkandarasi huyo hajapatikana kulieleza
hilo wakati huu ambapo uokoaji unaendelea kwa kutumia vikosi mbalimbali
vya ulinzi na usalama.
Majeruhi hao 15 walipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
matibabu huku wawili kati yao hali zao zikiwa mbaya. Pia magari madogo
manne yalipondeka baada ya kufukiwa na kifusi.
Tukio hili limetokea wakati serikali ikiwa bado haijachukua hatua za
kurekebisha kasoro zilizobainishwa na tume iliyoundwa na Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa baada ya kuporomoka kwa ghorofa la
Chang’ome Village Hoteli Inn mwaka 2006 na kuua mtu mmoja.
Tume hiyo ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam
yalikuwa yamejengwa kinyume na taratibu za ujenzi. Kati ya maghorofa
505 ambayo waliyakagua, 147 yalikutwa hayana nyaraka za ujenzi.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia Bunge kuwa tume hiyo ya Lowassa
ilibaini kuwa katika ukaguzi huo pia maghorofa 81 yalikutwa yamekiuka
masharti ya ujenzi huku mengine 22 wenyewe hawakupatikana na yalikuwa
yamejengwa bila kuzingatia sheria za ujenzi.
Hali ilivyokuwa
Tanzania Daima lilifika eneo la tukio majira ya saa 2:49 asubuhi na
kukuta hatua za awali za uokoaji zikiendelea na baada ya muda viongozi
mbalimbali waliwasili pamoja na vikosi vya uokoaji.
Vikosi mbalimbali vya polisi wakiwa na mbwa pamoja na farasi
vilizingira eneo hilo kuimarisha ulinzi na baadaye vikosi vya Jeshi la
Wananchi (JWTZ) na lile la Kujenga Taifa (JKT) viliwasili.
Majira ya saa 6:45 mchana, Rais Jakaya Kikwete akiambatana na mkewe
Salma Kikwete walifika huku kiongozi huyo akionekana mwenye hasira
ingawa hakuzungumza chochote zaidi ya kuangalia na kuondoka.
Baadaye kupitia Kurugenzi yake ya Mawasiliano Ikulu, rais alitoa
maagizo akizitaka taasisi za kitaaluma zinazohusika na shughuli za
ujenzi, wachoraji majengo, wakadiriaji majengo, wajenzi, makandarasi na
wahandisi nazo zichunguze tukio hilo kwa haraka.
Alisema baada ya kubaini yapi yalikuwa ni matatizo, zichukue hatua kwa mujibu wa madaraka na mamlaka yao.
Rais Kikwete pia aliwapa pole wafiwa pamoja na majeruhi wanaoendelea
kupatiwa matibabu baada ya kubanwa katika kifusi, wakiwamo watoto
wadogo ambao walikuwa wanacheza chini ya jengo.
Alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa Saidi Mecky Sadik pamoja na Kamanda
wa Kanda Maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova
kuhakikisha mjenzi wa jengo hilo, Mhandisi mshauri aliyekuwa anasimamia
ujenzi, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam aliyetoa kibali cha ujenzi
na pia Mkaguzi wa ujenzi pamoja na mwenye jengo wanapatikana haraka na
kuwajibishwa.
Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, mmiliki wa jengo hilo alikuwa tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi.
Kamanda Kova alisema hadi sasa kuna baadhi ya viongozi wa Manispaa ya Ilala wanashikiliwa kwa mahojiano ya awali.
Viongozi hao ni Mhandisi Mkuu wa Manispaa hiyo, Ogare Salu, Mkaguzi
wa Majengo, Wilbrod Bulyabuso na Mhandisi Goodluck Mbaga.
Kova alisema kuwa Mbaga alikuwa akihusika katika kulikagua jengo hilo mara kwa mara.
“Lakini nataka mtambue kuwa hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha
kuwa jengo hilo limejengwa chini ya kiwango, hadi wataalamu watakapotoa
taarifa baada uchunguzi wao,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadik alisema hali ya uokoaji
ilikwenda taratibu kutokana na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni
inayojenga jengo hilo kukosekana kutokana na jana kuwa mapumziko.
“Madereva wa mitambo kwa ajili ya uokoaji hawakuweza kupatikana pia
kupata taarifa muhimu kuhusu ni wafanyakazi wangapi walikuwemo ndani
wakati jengo hilo linaporomoka,” alisema.
Walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa kulikuwa na watu wengi kwani ilikuwa ni siku ya kumwaga zege.
Naye Aliridha Viranj (12) aliyeokolewa akiwa salama alisema kuwa alikuwa na watoto wenzake wapatao 13 wakicheza mpira.
“Wakati naondoka kabla sijafika mbali nikasikia sauti kubwa na mara
vumbi likatanda eneo zima, nikarudi tulipokuwa tunacheza na kumkuta
kaka yangu akiwa pembeni ameumia na ndipo wakaja watu na kuwasaidia,
wenzangu wengine watano na kuwapeleka hospitali,” alisema.
Aliwataja waliosalia ambao bado hawajatoka kuwa ni Yusuf Khaki, Suhail Karim, Zahid Abbas Kanji na Salmin Damji.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:
Post a Comment