Mbunge wa Chambani (CUF),marehemu Salim Hemed Khamis akiwa amebebwa na baadhi ya wabunge na watumishi wa Bunge baada ya kuanguka ghafla wakati akihudhuria vikao vya kamati za Bunge juzi.

Mbunge wa Chambani (CUF), Salim Hemed Khamis (60) amefariki dunia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa baada ya kuanguka ghafla juzi kwenye Ofisi za Bunge, Dar es Salaam.

Kifo cha mbunge huyo kimewagusa wengi akiwamo Rais Jakaya Kikwete ambaye ametoa ndege yake ili kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Pemba. Ofisi ya Bunge imethibitisha kutokea kwa kifo hicho cha mbunge huyo na kueleza kuwa, alipatwa na ugonjwa wa kiharusi uliosababishwa na ugonjwa wa moyo (Hypertension).

Khamis anatarajiwa kusafirishwa kisha kuzikwa leo kijijini kwao Chambani, Pemba baada ya jitihada za kumsafirisha jana kushindikana na wabunge wengi kuomba kushiriki kumuaga.


Mbunge huyo atasafirishwa leo saa tatu asubuhi baada ya shughuli ya kuaga itakayofanyika kwenye Viwanja vya Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Anne Makinda ametangaza kusitishwa kwa shughuli zote za Kamati za Bunge hadi Jumanne Aprili 2, kutokana na msiba huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Makinda alisema: “Ninatoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Chambani, Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, wabunge wote na Watanzania wote kwa jumla”.

Khamis alianguka juzi saa 10.50 asubuhi wakati akishiriki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kilichofanyika katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko ambacho kilisababishwa na kupasuka kwa mshipa wa damu kichwani.

“Tumeelezwa na daktari kuwa Mbunge Salim amefariki kutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ambayo ilimiminikia kwenye ubongo wake na kuenea kichwani,” alisema Joel. Alisema kutokana na hali hiyo shughuli zote za uchambuzi wa bajeti zilizokuwa zikifanywa na kamati za Bunge, zimeahirishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo hadi tutakapomaliza shughuli za mazishi.

Joel alisema kwa upande wa Bunge, shughuli za msiba zitaongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ambayo marehemu alikuwa mjumbe.

Alisema Bunge linamshukuru Rais Kikwete kwa kutoa ndege yake kwa ajili ya kupeleka mwili huo Pemba na kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa wabunge wengi kushiriki mazishi. Alisema kutokana na hali hiyo wabunge 12 wakiongozwa na Lowassa watakwenda kushiriki kwenye msiba.

Wabunge, CUF waomboleza
Baadhi ya wabunge jana walionekana kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa za msiba huo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa kifo hicho ni cha ghafla kwa sababu Salim alikuwa kwenye vikao vya Bunge tangu walipoanza vikao vya kamati.

“Tangu tuanze vikao vya kamati tulikuwa naye na alionekana kuwa mwenye afya, kwangu mimi ni pigo nimepata kwa sababu alikuwa mwalimu kisiasa katika Chama cha CUF,” alisema Rajab Mohamed Khamis, ambaye ni Mbunge wa Ole (CUF).

Kwa upande wake, Mbunge wa Peramiho CCM, Jenister Mhagama alishtuka na kuonekana kutoamini taarifa hizo, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kuzungumza chochote.


Wabunge wengi walionekana wakihaha kutafuta usafiri ili waweze kwenda Muhimbili huku baadhi yao wakienda kujiandaa na safari ya kwenda Pemba.

Chanzo: Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top