Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda
MAWAZIRI wawili wa Rais Jakaya Kikwete, jana walionja ‘joto la
jiwe’ baada ya wananchi wa Mtwara kuwazomea mkutanoni na hivyo
kulazimika kukatiza mkutano wao.
Mawaziri hao ni Dk. Abdallah Kigoda wa Wizara ya Viwanda na Biashara
na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, waliokuwa wameongozana na
Balozi wa Nigeria hapa nchini, Nshaya Manjabu, na Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Dangote ya Nigeria, Deva Kumar.
Tukio hilo limekuja zikiwa ni wiki chache tangu kutokea kwa vurugu
kubwa mkoani humo katika wilaya za Mtwara Mjini na Masasi ambapo
wananchi waliharibu mali za baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali na
kumuua askari mmoja huku watu wengine wanne nao wakiuawa kwa kupigwa
risasi.
Wananchi hao wa Mtwana na Lindi wamekuwa na msimamo mkali wakipinga
serikali kujenga bomba la kusafirisha gesi asili kutoka kwao kwenda
jijini Dar es Salaam bila kuwekewa mazingira mazuri ya kiuchumi.
Katika kuonyesha kuwa wananchi hao walikuwa wamepania kuwasulubu
mawaziri hao, walifika mkutanoni huku baadhi yao wakiwa na mabango
yaliyokuwa na ujumbe wa kuhoji mkutano huo umeruhusiwa na nani wakati
serikali imepiga marufuku mikutano na maandano mkoani humo kwa muda.
Mara baada ya viongozi hao kufika uwanjani, Waziri Kigoda aliwasalimia wananchi akisema: “Mtwara oyeee!!!”
Waziri huyo aliitikiwa na wananchi: “Haitoki hata kama umekuja wewe
hatutaki wala hatukuelewi! Mlikuwa wapi kuja huku mapema kutuelewesha
habari za viwanda?”
Wanachi hao walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe uliosomeka: “Kauli
mbiu: gesi haitoki, tunashukuru baada ya kimya kirefu sasa leo mmefungua
rasmi mikutano tukianzia huu mkutano wenu na gesi ndio roho yetu.”
Wakati ‘zomeazomea’ hiyo ikiendelea, baadhi yao walianza kurusha mawe
katika hali iliyowalazimu viongozi kuufunga mkutano huku Jeshi la Polisi
likiamuru wananchi kutawanyika katika viwanja vya mkutano.
Mara baada ya hali hiyo ya vurugu, Naibu Waziri wa Uchukuzi
alilazimika kuwatuliza wananchi ili wasikilize akisema: “Nisikilizeni
mtaelewa tu, mwekezaji amepatikana na amemaliza hatua ya kwanza ya
kufanya makadilio ya gharama za ujenzi.”
Aliongoza kuwa mamlaka ya viwanja vya ndege inafanya mazungumzo naye
ili masharti ya uwekezaji yaweze kufahamika na upanuzi wa uwanja kuanza
mapema.
Hata hivyo, wananchi hao hawakutulia huku wakiendelea kupiga kelele na
kuwazomea: “Hilo ni changa la macho, hatutaki propaganda zenu,
tumechoka na siasa zenu.”
Mkuu wa Mkoa Mtwara, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, hakupata nafasi
ya kuzungumza kutokana na wananchi hao kuzomea huku wakimtaka aondoke.
Awali, Kigoda akizungumza katika viwanja vya bandari ya Mtwara na
watumishi mbalimbali, alisema kuwa lengo la ujio wake mkoani humo ni
makabidhiano ya makontena 38 ya vifaa vya ujenzi wa kiwanda cha saruji
cha Dagonte kinachotarajiwa kujengwa katika kijiji cha Msijute, wilaya
ya Mtwara vijijini.
Makabidhiano hayo yalikuwa kati yake na Naibu Waziri wa Uchukuzi.
Pamoja na mambo mengine, Kigoda alisema kuwa serikali itaendelea kupokea
wawekezaji mbalimbali watakaoomba kuwekeza katika mkoa huo.
Alisema wanaangalia zaidi uwekezaji katika ujenzi wa viwanda kwa kuwa
Mtwara ni kitovu cha uchumi wa taifa huku akisisitiza kuwa utafiti wa
kitaalamu na kisayansi unaonyesha gesi hapa Mtwara ni nyingi sana.
Alisema viwanda vingi vitajengwa hapa na gesi itakayobaki lazima itapelekwa katika maeneo mengine.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment