STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21 Februari,2013
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesisitiza dhamira ya dhati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii Zanzibar kwa kushirikiana na
washirika wa sekta hiyo ikiwemo sekta binafsi.
Dk
Shein ametoa kauli hiyo leo Ikulu wakati wa mazungumzo na Bodi ya
Wakurugenzi wa Jumuiya ya Wawekezaji katika Sekta ya utalii Zanzibar
(ZATI) na Jumuiya ya Makampuni ya Watembeza Watalii Zanzibar (ZATO).
“Dira
yetu ya maendeleo ya mwaka 2020 inatuelekeza kuwa utalii ndio sekta
mama na halikadhalika Mpango wetu wa Kupunguza Umasikini Zanzibar-MKUZA
II umetilia mkazo sio tu nafasi ya sekta ya utalii katika kupambana na
umasikini bali pia maendeleo yetu kwa ujumla” alisema Dk. Shein.
Katika
mnasaba huo Dk. Shein alizipongeza Bodi na viongozi wa ZATI na ZATO kwa
ushirikiano wao kwa Serikali na Taasisi zake kama vile Kituo cha
Uwekezaji Zanzibar-ZIPA, Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA na Bodi ya Mapato Zanzibar-ZRB ushirikiano ambao aliueleza kuwa umesaidia sana kukuza sekta hiyo Zanzibar.
Alibainisha
kuwa madhumuni ya kuleta dhana ya utalii kwa wote ni kuhakikisha kuwa
kila mmoja anashiriki kwa nafasi yake na mahala alipo kwa namna moja au
nyingine katika kukuza na kuimarisha utalii Zanzibar.
“Tunataka
kila mtu ashiriki kukuza na kuimarisha utalii kwa sababu ndio sekta
yetu kuu ya uchumi na inatufaidisha sote kwa namna moja au nyingine”
alifafanua Dk Shein.
Katika
mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Mshauri wa Rais masuala ya
Utalii Ndg. Issa Ahmed, ujumbe wa ZATO na ZATI walibadilishana mawazo na
Rais kuhusu masuala ya huduma katika sekta ya utalii, usalama wa
watalii, kuitangaza Zanzibar nje kuvutia uwekezaji na kuongeza idadi ya
watalii pamoja na haja ya kuimarisha mafunzo kwa wananchi wa Zanzibar
ili kuongeza ajira kwa wazanzibari katika sekta hiyo.
Kwa
hiyo alitoa wito kwa wadau wote katika sekta ya utalii na zile ambazo
zinahusiana na sekta hiyo pamoja na wananchi kushirikiana kwa hali na
mali kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo
muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia
washirika wa sekta ya utalii kuwa milango ya Serikali yake iko wazi kwa
majadiliano ya mara kwa mara kuhusu namna bora ya kuimarisha sekta ya
utalii nchini.
Katika
mazungumzo hayo ujumbe wa ZATI uliongozwa na Mwenyekiti wake Ndg.
Abdulswamad Said Ahmed na ule wa ZATO uliongozwa na Mwenyekiti wake Ndg.
Khalifa Mohamed Makame.
Said Ameir, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment