Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dkt. Norman Sigala (Mwenye tai) akipata maelezo kutoka kwa mkuu wa shule ya Sekondari Santilya  juu ya ujenzi wa jengo la nyumba ya mwalimu ambalo bado halijakamilika ingawa fedha zilitolewa.

Hili ni jengo la nyumba ya mwalimu ambalo bado halijakamilika ingawa fedha kwa ajili ya ujenzi wake zilitolewa.
Mkuu wa Wilaya Dkt. Sigala akihutubia wanachi jana, 20 Februari 2013 katika Shule ya Sekondari Santilya Mbeya Vijijini.

 Wanafunzi na wananchi wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mkuu Wilaya ya Mbeya Dkt. Norman Sigala. Kwa mbele, kuanzia kulia,  ni majengo mawili yenye jumla ya vyumba vinne kati ya sita ambavyo havitumiki katika Shule ya Sekondari Santilya.

Serikali imesema haitawavumilia wakuu wa shule ambao watabainika kutumia vibaya fedha zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule.


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dkt. Norman Sigala alipokuwa akizungumza na wananchi na wanafunzi katika shule ya Sekondari Santilya iliyopo Mbeya Vijijini wakati wa ziara ya kukagua shughuli za maendeleo katika shule hiyo.


Mkuu huyo wa wilaya amemtaka mkuu wa shule aliyekabidhiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu afike ofisini kwake ili aeleze kiasi cha fedha alichopewa na sababu za jengo kutokamilika hadi sasa.

 “Sijafurahishwa na jengo la mradi wa MESS ambalo bado halijakamilika hadi sasa ingawa fedha zilitolewa hivyo naagiza mkuu huyo popote alipo aambiwe ili afike ofisini kwangu aeleze alivyotumia fedha alizopewa kwa ajili ya jengo hili”. Alisema Dkt. Sigala.

Mkuu wa shule aliyekabidhiwa fedha za ujenzi wa jengo hilo iliripotiwa kuwa amehamishiwa katika shule ya Sekondari Iwambi jijini Mbeya.
 

Aidha, Dkt. Sigala aliwapongeza wananchi kwa kujenga madarasa ya kutosha kiasi cha kuwa na madarasa ya ziada sita na kuwaagiza kuwa kwa sasa waelekeze nguvu zaidi kwenye ujenzi wa nyumba za waalimu na serikali itachangia bati kwa kuwa waalimu hawana nyumba za kuishi.

 “Kusanyeni nguvu, mkijenga nyumba za waalimu hadi kiwango cha mtambaa panya hata zikiwa kumi njooni ofisini kwangu mtapata bati”. Alisema Dkt. Sigala.


Akizungumzia tatizo la uhaba wa waalimu, mkuu huyo wa Wilaya amekemea tabia ya baadhi ya wakuu wa shule kutotaka kufundisha hata kama wamesomea masomo ambayo hayana waalimu katika shule zao. Hivyo, amewaasa kufundisha baadhi ya vipindi badala ya kubaki ofisini tu.


Awali Mwananchi aitwaye Amani Mbeyale aliomba kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ufafanuzi wa tatizo la uhaba wa waalimu katika shule ya Sekondari Santilya ambapo alisema waalimu ni wachache na waliopo, wengi wao, wanafundisha masomo yanayofanana.

Aidha, Dkt. Sigala aliwaasa wanafunzi kujijengea tabia ya kupenda kusoma masomo ya sayansi tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi hukimbilia masomo ya sanaa.


Vilevile Dkt. Sigala amewaasa wanafunzi  kuachana na tabia ya kujiingiza kwenye maswala ya mapenzi kwa vile kufanya hivyo ni kupoteza muda wao wa shule na kujiharibia maisha yao.

 “shule sio mahali pa kujifunzia mapenzi kwani kushiriki katika mapenzi ni hatari kwa mwanafunzi” Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.


Amewataka wazazi kuonesha ushirikiano katika kukomesha tabia ya wanafunzi wa kike kujiingiza katika mapenzi kwa kuwataja wanaoshiriki kuwadanganya badala ya kungoja wapate mimba  ndipo waanze kulaumiana.


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top