Na Edna Bondo
WAKATI watanzania wengi hawajasahau machungu ya kulizwa na kampuni ya kupanda na kuvuna mbegu ya DECI, kumeibuka taasisi mpya ya fedha inayojitapa kutoa mikopo kwa njia ya mtandao, huku ikitumia vibaya majina ya Rais Jakaya Kikwete na Barack Obama wa Marekani.

Mbali ya taasisi hiyo ya Tanzania Loans Society kutumia majina ya marais hao, imewahusisha pia Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Ridhiwani Kikwete, ambapo inahofiwa kutapeli mamilioni ya walalahoi.

Taarifa za taasisi hiyo zinaonesha kuwa ilianza shughuli zake mwaka 2012, na kupata ufadhili wa fedha kutoka kwa Rais Obama, ambapo inasimamiwa na Rais Kikwete, Waziri Mkuu Pinda na mratibu mkuu ni Ridhiwani.

Watendaji wengine ni Michael John ambaye namba yake ya simu ya mkononi ndiyo inayotumika kutuma pesa za usajili.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa taasisi hiyo, imekuwa ikijitangaza kutoa huduma ya mikopo na mawasiliano ya jinsi ya kupata mikopo hiyo, hufanyika kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha wateja wa mikoani kupata mikopo hiyo kirahisi bila usumbufu wa kuja makao makuu yao jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi walioomba kupata mikopo hiyo, waliliambia gazeti hili kuwa, fomu za mikopo ya taasisi hiyo hutolewa kwa sh 15,000 ambazo nazo hulipiwa kwa njia ya mtandao.

Mmoja wa wateja wa taasisi hiyo aliyedai kutapeliwa, Maywood Maganga alisema alionja machungu baada ya kuingia kwenye tovuti yake na kukutana na maelekezo ya kumtaka ajaze fomu na taarifa zake binafsi na kisha kutakiwa kutuma sh 15,000 kwenda kwenye namba 0656 73 64 16, iliyosajiliwa kwa jina la Michael John.

Maganga alisema kuwa alifanya hivyo, na kusubiri majibu.
Kwa mujibu wa mkopo huo wenye masharti nafuu, tena usio na riba, mteja hutakiwa kurejesha na kuanza kukatwa baada ya miezi miwili tangu siku ya kupokea pesa hizo za mkopo.
“Maelezo ya mkopo huo yanaonesha kuwa una masharti nafuu sana na marejesho yake ni sh 60,000 kila mwezi bila kujali kiasi ambacho mteja amekopa.
“Maelezo ya fomu niliyojaza yalinionesha kwamba nitapata sh 300,000 kama zawadi kwa kukubali kukopa na baada ya dakika 30, ningeingiziwa kiasi cha fedha za mkopo nilizoomba,” alisema.

Kwa mujibu wa Maganga, fomu alizozikuta kwenye tovuti ya taasisi hiyo, zilionesha mahala ofisi ilipo, lakini alipofuatilia na kuuliza, alibaini kuwa taasisi hiyo haina ofisi katika jengo la serikali la Utumishi wa Umma.
“Mwanzoni sikuwaza kama taasisi hii itakuwa ya kitapeli, lakini baada ya siku mbili ya kutokutumiwa pesa hiyo ndipo nilipogundua kwamba nimetapeliwa,” aliksema.

Maganga aliziomba mamlaka husika kuingilia kati kwa kudhibiti utapeli huo, kwani Watanzania wengi wameshalizwa kupitia taasisi hiyo inayotumia majina ya watu maarufu kutapeli.

Aidha, maelezo ya tovuti hiyo yanaeleza zaidi kuwa kwa kutambua ugumu wa maisha uliopo kwa Watanzania na kukua kwa teknolojia kama nchi zingine zifanyavyo, taasisi hiyo inatoa mikopo kwa njia hiyo ya mtandaao ili kuepuka usumbufu wa kuwafikia watu walioko mikoani ili nao wanufaike.

Mbali ya hayo, pia taarifa ya maelezo ya taasisi hiyo hiyo ilieleza kuwa kiwango cha chini cha kupata mkopo ni sh 100,000 na ofisi zake zipo katika jengo la utumishi wa umma, ghorofa ya tano chumba namba 30.

Ridhiwani hakuweza kupatikana kuzungumzia taasisi hiyo, lakini katika taarifa aliyoituma hivi karibuni kwenye ukurasa wake wa facebook, alikanusha yeye na viongozi wa serikali akiwemo Rais Kikwete kuhusika na taasisi hiyo.
“Maisha ni kuhangaika na kwamba inataka mtu anayefahamu njia sahihi kuweza kujua kuwa nikitumia njia hii hali itakuwa sawa na pengine mambo yangu yatanyooka.
“Hii inaweza kuwa ndiyo maana halisi ya kuhangaika ufanikiwe, lakini tafsiri hii haiwezi kuwa kutumia njia za kudhulumu, kukaba, kuiba au kufanya utapeli ili ufanikishe malengo yako mabaya dhidi ya mtu au kikundi fulani cha watu," aliandika Ridhiwani kwenye ukurasa wake wa facebook.

Kwa mujibu wa Ridhiwani, hivi karibuni alipokea ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya mkononi na barua pepe, ikihoji kuhusika kwake na kampuni hiyo.

Alisema mradi huo unadaiwa kuanzia katika mikono ya Rais Obama kuja Tanzania kupitia Kikwete na sasa yeye akishirikiana na Waziri Mkuu Pinda wanauendesha.

“Jambo hili si la ukweli hata kidogo, na naomba kutumia nafasi hii kulikanusha kabisa mbele ya umma wa Watanzania na wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wanafuatilia,” ilisema taarifa hiyo ya Ridhiwani.

Vilevile taarifa ya Ridhiwani ilitahadharisha umma wa Watanzania kuwa makini na mambo ya mitandao ambayo hutumia jina lake kwa utapeli kwa lengo la kumchafua, lakini yeye na viongozi wengine hawahusiki na Tanzania Loans Society.

Viongozi wa taasisi hiyo hawakuweza kupatikana kwa njia yoyote ile kwani simu zao hazipokelewi na hata katika ofisi wanazodai kuwapo, hawaonekani. 
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top