Na Farida Ramadhani
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
KINARA wa vurugu za kidini zinazoibuka kila siku ya Ijumaa jijini Dar es Salaam, amejulikana.
Kinara huyo ametajwa kuwa ni Sheikh Issa Kondo Bungo ambaye amekuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu bila mafanikio.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
zilisema kuwa Sheikh Bungo anadaiwa kuhusika na matukio kadhaa makubwa
ya vurugu za kidini, zilizotokea kwa nyakati tofauti jijini Dar es
Salaam.
Duru za kipolisi zilitaja baadhi ya matukio ambayo Sheikh Bungo
anadaiwa kuhusika nayo kuwa ni pamoja na tukio la kuchoma moto kanisa la
TAG la Mbagala, baada ya mtoto (jina limehifadhiwa), kukojolea Qur’an.
Tukio la kukojolea kitabu hicho lilitokea Oktoba 10 katika eneo la
Chamazi saa 10 jioni wakati watoto hao wakiwa katika ‘kijiwe’ chao cha
kuchezea mpira.
Vurugu hizo zilisababisha kuvunjwa kwa vioo vya magari, madirisha ya
makanisa pamoja na kuibwa kwa vifaa vya kwaya katika makanisa hayo
ambayo ni ya Anglikana, Wasabato na Pentekoste.
Kutokana na tukio hilo ambalo liliibua vurugu kubwa kutoka kwa baadhi
ya waumini wa Kiislamu wanaojiita wenye msimamo mkali, Sheikh Bungo
anatajwa kuhusika kushawishi wenzake kuchoma kanisa hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Jeshi la Polisi limekuwa likimsaka kwa
muda mrefu, lakini halijafanikiwa kumtia mbaroni kutokana na staili yake
ya kuishi kwani hana makazi maalumu.
“Shekh huyo pia anahusika kushawishi wafuasi wa Katibu wa Jumuia na
Taasisi za Kiislamu Ponda Issa Ponda kuandamana kila siku ya Ijumaa ili
kushinikiza mahakama itoe dhamana kwa Ponda ambaye kwa sasa yuko rumande
akikabiliwa na kesi ya uchochezi,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kwa mujibu wa habari hizo, tangu tukio la vurugu za Mbagala
lilipotokea, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata wafuasi wa sheikh
huyo na wengine wako mahakamani, lakini yeye hajapatikana.
Tayari Sheikh Bungo pamoja na wenzake wamefunguliwa kesi namba THA/ IR/ 7794/ 2012 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
“Mwaka huu tumeshamfungulia jalada lingine namba CHA/ RB/ 10652013
katika kituo cha polisi cha Chang’ombe, hivyo tunawaomba wananchi
wanaopenda amani watoe taarifa katika kituo chochote cha polisi endapo
ataonekana,” alisema mtoa habari wetu.
Hadi sasa polisi imemfikisha mahakamani Shekh Ponda pamoja na wenzake
49 ambao kesi zao zinaendelea kusikilizwa huku wakiendelea kukamata
wengine kila vurugu hizo zinapotokea.
Vurugu hizo ambazo zimekuwa zikiwatia hofu wakazi wengi jijini Dar es
Salaam na nchi nzima kwa ujumla, zimekuwa na tabia ya kuibuka kila siku
ya Ijumaa na siku ambazo kesi ya Sheikh Ponda inapotajwa.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya shughuli za kimaendeleo
katika jiji hilo kusimama kwa muda, huku polisi wakilazimika kutumia
nguvu kubwa kuweka ulinzi.
VIA: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment