Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania John Tendwa

Vyama vya siasa vimetakiwa kujipanga vyema kwa ajili ya uchaguzi ili kupata matokeo mazuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ule wa serikali za mitaa mwaka 2014.

Msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa amesema viongozi wa vyama hivyo wanatakiwa kuwa na utashi wa kisiasa kwa kujenga umoja miongoni mwao na kujenga utamaduni wa kutumia ushawishi badala ya vurugu

Msajili huyo amesema vyama vya upinzani vinatakiwa kuikosoa serikali kwa misingi ya sheria ili iweze kutekeleza mipango ya maendeleo kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika kila uchao kuhusiana na masuala mbalimbali.

 katika hatua nyingine  Bwana Tendwa amesema kuwa sheria ya uchaguzi inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuruhusu vyama vya SIASA kuungana katika kugombea nafasi fulani kama urais au ubunge kwa ajili ya ustawi wa demokrasia hapa nchini.

Kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi,Msajili amesema ni sheria muhimu kwa ajili ya maadili ya viongozi na pia kupunguza vitendo vya rushwa kwani viongozi wakipatikana kwa njia ya Rushwa wanaweza kuingia katika vitendo vya kifisadi ili kurejesha fedha walizotumia nyakati za uchaguzi.

Msajili huyo amezitaka taasisi za kisiasa kuwa huru katika kutoa maoni ya katiba kwani kila mwananchi na jumuiya mbalimbali zina uhuru wa kuchangia kwa mujibu wa sheria na haki za binadamu.

Tanzania imetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa siasa wa vyama vingi mwaka 1992 ambapo vyama vilivyoanza vilikuwa 13 lakini vimeongezeka kufikia   vyama 20  mpaka sasa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top