Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Tanzania na Ufaransa zimekubaliana kuwa na mpango mwingine wa miaka mitatu ambako Ufaransa itasaidia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya huduma ya kijamii ikiwamo ile ya upatikanaji kwa maji safi na salama.
Hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ufaransa (AFD) Bwana DovZerah mjini Paris, Ufaransa ambako  Rais Kikwete amemaliza ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku tatu.
Aidha, nchi hizo mbili zimekubaliana kuwa makubaliano hayo mapya yalenge katika kuelekeza nguvu na raslimali hizo za maendeleo katika sekta chache, mbili ama tatu, ili raslimali hizo ziweze kutumika vizuri na matokeo yake kuonekana badala ya kusambaza raslimali hizo kwa sekta na maeneo mengi.
Mara baada ya kumshukuru Bwana DovZerah kwa mchango mkubwa wa Ufaransa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitatu kati ya 2006 na 2010, Rais Kikwete amependekeza kuanzishwa kwa mpango mpya, jambo ambalo Mkurugenzi Mkuu huyo amelikubali mara moja.
Rais Kikwete pia amependekeza kuwa raslimali katika mpango huo mpya zielekezwe katika sekta na maeneo machache, mawili ama matatu, ili raslimali hizo ziweze kutumika kwa mafanikio makubwa zaidi na matokeo yaonekane waziwazi.
Chini ya mpango wa  kwanza  ambako Ufaransa iliipatia Tanzania kiasi cha dola za Marekani 50.9 nguvu zilielekezwa katika kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama katika miji ya Utete na Mpwapwa na katika miji midogo inayozunguka Ziwa Victoria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top