SAKATA la gesi sasa limeingia hatua mpya, baada ya watendaji wakuu wa CCM; Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kuitaka Serikali ikae na wana-Mtwara ili kuona namna ya kumaliza mgogoro huo kwa amani.

Kinana na Nape walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti jana. Wakati Kinana alisema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Nape alifanya hivyo kupitia mtandaowa Twitter na baadaye kuthibitisha kauli hiyo alipoulizwa na mwandishi wetu.

Wakati watendaji hao wa CCM wakitoa matamko hayo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanya vikao mfululizo mkoani Mtwara akisaka suluhu ya mgogoro huo.

Kinana na Nape
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Ofisi za CCM Wilaya ya Uvinza, Kigoma, Kinana aliitaka Serikali isikilize hoja za wakazi wa Mtwara na kuzitafutia usumbufu sahihi.

Mbali na kutoa ushauri huo, aliitaka pia Serikali kuwasaka watu wanaochochea mgogoro huo kwa kufanya vurugu na kuharibu mali za watu na kuwafikisha mbele ya sheria.
“Serikali ikae na wana-Mtwara na kuwasikiliza, wananchi hao wana hoja na Serikali inapaswa kutoa majibu sahihi kwa hoja hizo. Lakini pia iwasake na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha uvunjifu wa amani,” alisema Kinana.

Kwa upande wake, Nnauye aliitaka Serikali kuwasikiliza wananchi wa Mtwara kwa kuwa madai yao ni ya msingi... “Wakazi wa Mtwara na Lindi wanazo hoja za msingi juu ya suala la gesi, hoja ambazo ni muhimu kusikilizwa na kupatiwa majibu sahihi.”

Nape alisema hoja za wakazi hao ni za msingi lakini akaongeza kuwa kuna baadhi ya wahuni ambao wanatumia mwanya huo kupora na kuharibu mali za watu. “Kuna uhusiano gani kati ya hoja yao ya madai ya gesi na kuchoma nyumba za watu, kuharibu mali za umma na magari ya watu. Kuna kundi la wahuni ambalo Serikali inatakiwa kuhakikisha inapambana nalo na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” alisema Nape.


Pinda asaka suluhu
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alikuwa na kibarua kizito kusaka suluhu ya mgogoro wa gesi baada ya kuzungumza na makundi mbalimbali ya kijamii kupata mawazo yao.

Pinda aliyeongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja alianza kazi hiyo juzi kwa kufanya vikao vya ndani na viongozi wa Serikali mkoa wa Mtwara. Habari kutoka Mtwara zinaeleza kuwa kutwa nzima ya jana, Waziri Mkuu Pinda alikuwa akifanya mikutano mbalimbali na makundi kadhaa kwa lengo la kupata suluhu ya mgogoro huo wa gesi.

“Alianza kwa kufanya mazungumzo ya ndani na viongozi wa dini, wanaharakati, wanasiasa na baadaye viongozi wa Serikali za Mitaa,” kilieleza chanzo cha habari kutoka Mtwara.
Mbali na viongozi hao, Pinda pia alizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa CCM na madiwani kabla ya mkutano wake na waandishi wa habari aliopanga kuufanya baadaye jioni.
Mmoja wa madiwani waliohudhuria mkutano huo wa Pinda alilieleza gazeti hili kuwa, Waziri Mkuu aliwaambia kuwa mkutano wake huo ni kwa ajili ya kukusanya maoni.

“Amesema amekuja kukusanya maoni na baadaye atakwenda kushauriana na Rais Jakaya Kikwete na atatoa tamko kuhusu hatima ya suala hilo baadaye,” alisema diwani huyo akimnukuu Waziri Mkuu Pinda.


Gesi kuteka Bunge
Mkutano wa Kumi wa Bunge unaanza leo mjini Dodoma, huku suala la gesi likitarajiwa kutawala mijadala mbalimbali ya wabunge.

Via Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top