Rais Jakaya Mrisho Kikwete |
Mhe. Rais pia
amezishukuru na kuzipongeza taasisi za umma na binafsi zinazoshiriki katika
kuufanikisha mradi huo unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs
Conservation Project.
"Juhudi hizi za
kurudisha tena makundi ya mbwa mwitu kwenye mbuga hii inayojulikana kimataifa ni ya kupongezwa kwani itahakikisha
kwamba wanyama hawa wanaendelea kuwepo Serengeti na pia itaongeza idadi ya vivutio vyetu vya utalii mbugani humu", alisema Mhe. Rais
Aliyasema hayo Jumapili Desemba 23, 2012 wakati wa sherehe
za kuachiwa huru kundi la pili lenye
mbwa mwitu 15 waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi kadhaa kwenye boma maalumu la
mradi huo, lililojengwa katika eneo la
Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
"Nashukuru
taasisi zote zinazounga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba mbwa
mwitu wanakuwepo kwa wingi mbugani
Serengeti kama ilivyo katika mbuga zingine", aliongezea Mhe. Rais.
Katika taarifa yake
wakati wa sherehe hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alimueleza
Rais Kikwete kuwa jumla ya Mbwa mwitu ishirini na sita (26), wamerudishwa
mbugani hadi sasa, kufuatia kundi la
kwanza la wanyama mwitu hao kumi na moja (11) kuachiwa siku ya Alhamisi Agosti
30, 2012.
Alitanabahisha
kwamba mradi huo unaohusisha mbwa mwitu walioondolewa katika msitu wa
Samunge wilayani Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya
wanyama hao katika mbuga hiyo maarufu duniani, na kwamba baada ya kuhifadhiwa
na hatimaye kuachiwa kwao huku wakiwa wamevishwa collar maalumu zenye redio ili kufuatilia nyendo
zao, ni muendelezo wa juhudi za kupata
makundi sita yenye mbwa mwitu takriban kumi (10) kila moja, ikiwa ni hatua
endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha
uwepo wa wanyama hao mbugani humo.
Dkt. Mduma
alisema kundi la kwanza la mbwa mwitu
hao kumi na moja (11) wote wapo hai na wanaendelea vizuri katika maisha yao
mbugani humo, na kwamba pamoja na wanyama hao kutembelea hadi maskani yao ya
awali ya Loliondo, malalamiko ya kuwapo kwa uharibifu wa mifugo sehemu hizo
kama ilivyokuwa awali hayajaripotiwa hadi sasa.
Mkurugenzi Mkuu huyo
wa utafiti wa wanyama pori alieleza kuwa mbwa mwitu wamekuwa wakitoweka
kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao, ama kwa kuugua
magonjwa mbalimbali kama vile kichaa cha mbwa.
"Hivi sasa kuna
makundi 11 yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya
Ngorongoro, yakifanya idadi ya mbwa mwitu kuwa 200", alisema Dkt Mduma.
Aliongezea kuwa awali,
katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti makundi ya mbwa mwitu yalikuwa yakionekana
kwa wingi, lakini yamekuwa yakitoweka kwa kasi sana kiasi hata mara ya mwisho ni wanyama mwitu hao wawili tu walioonekana katika mbuga ya Serengeti mnamo mwaka 1998.
Mbwa mwitu ni miongoni
mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani.
Takwimu zinaonyesha
kuwa katika Bara la Afrika kuna mbwa
mwitu takriban 8,000 na kwamba Tanzania pekee inakadiriwa kuwa na wanyama hao 3,500 katika mbuga mbalimbali
nchini, isipokuwa katika Hifadhi h ya
Taifa ya Serengeti ambako walianza kutoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha
kuanza.
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom imechangia dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha
miaka mitatu ili kufanikisha mradi huo, ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Julai
mwaka 2011.
"Vodacom
tunajisikia furaha sana kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha
sekta ya utalii ambayo kwa sasa mchango
wake ni mkubwa sana kwa taifa", alisema Bw. Salum Mwalimu,
Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom wakati wa sherehe za kuwarudisha mbugani mbwa
mwitu hao 15.
Bw. Mwalimu alisema
kampuni yake siku zote inalenga kubadili maisha ya watu na kwamba ni wazi
kuimarika kwa Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti inayochangia kwa kiasi kikubwa
sekta ya utalii nchini na ambayo inategemewa kwenye kuongeza pato la
Taifa na ustawi wa watu ni jambo muhimu sana.
Taasisi zingine
zinazoshiriki katika zoezi hilo ni Idara ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI),
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Frankfurt Zoological Society (FZS) , Grumeti
Fund (GF) na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Picha kutoka maktaba.
Picha kutoka maktaba.
0 comments:
Post a Comment