Waziri Mkuu Mizengo Pinda
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote kushiriki chanjo ya kuzuia kichomi na kuhara kwa watoto pindi itakapoanza kutolewa mapema mwakani.

Ametoa wito huo jana jioni (Jumanne, Desemba 25, 2012) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa kata ya Kibaoni na kata jirani za Ikuba, Usevya, Mbede, Mamba na Majimoto walioshiriki kula naye chakula cha mchana kuadhimisha sikukuu ya Krismasi.


Sherehe hizo zilifanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Kakuni ambako pia ni kijijini kwake kata ya Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi.


“Serikali itaanza kutoa chanjo ya kuzuia kichomi (kitaalam wanaiita pneumonia) na ya kuzuia kuhara. Magonjwa haya mawili yana madhara makubwa kwa watoto wadogo. Natoa wito kwa Watanzania wake kwa waume, wakati ukifika wapelekeni watoto kwenye hiyo chanjo ili kuokoa maisha yao,” alisisitiza.


Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakazi wa kata hizo kununua vyandarua na kuvitumia ili kujikinga na ugonjwa wa malaria kwa vile ndiyo unaoongoza kwa vifo nchini kuliko magonjwa mengine.


“Nawasihi wafugaji, ninyi mna hela… uzeni mifugo ili mpate fedha ya kununua chandarua, takwimu zinaonyesha kuwa kila baada ya dakika tano kuna mgonjwa anakufa kutokana na malaria. Kwa hiyo mtu akipata visenti vyake, anunue chandarua kwa mkewe na watoto,” alisisitiza.


Akizungumzia kuhusu UKIMWI, Waziri Mkuu alitaka wakazi wa jimbo lake la Katavi kutambua kwamba ugonjwa huo upo na kwamba hauna tiba na tena hauchagui kijana wala mzee, kijana wa kiume au wa kike.


“Ninachowasisitiza hapa ni kwamba mtambue kuwa kuwa ugonjwa huu upo tena hauna tiba. Kilichopo sasa ni dawa za kupunguza makali ya virusi ambazo zinasaidia kurefusha maisha. Ugonjwa huu hauchagui kijana wala mzee, hauchagui kijana wa kiume wala wa kike. Ni lazima tujihadhari,” alisisitiza.


Hivyo, aliwasihi waende kupima kwa hiari kwenye hospitali ya wilaya au wakati wa maonyesho ili waweze kujitambua hali zao na kufuata ushauri watakaopewa baada ya kupokea matokeo.


“Kama umeambukizwa utapewa ushauri wa namna ya kuishi, ukikutwa hujaambukizwa pia utaelezwa namna ya kuchukua tahadhari ili usipate maambukizi mapya,” alisema.


Kuhusu kilimo na ufugaji nyuki, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi wa kata hizo wafanye kazi kwa bidii na maarifa ili waweze kupata mabadiliko ya haraka katika kujiletea maendeleo yao kiuchumi.


Wakati huohuo, Waziri Mkuu aliahidi kumpatia mizinga mitatu ya kufugia nyuki, Bw. Julius Kansunko (55) baada ya kuibuka mshindi wa kusakata rumba katika sherehe hiyo. Pia aliahidiwa mizinga miwili na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Bw. Iddi Kimanta ambaye alikuwepo kwenye sherehe hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.


Bw. Kansunko alipata fedha taslimu sh. 40,000/- ambapo sh. 20,000/- zilitoka kwa Waziri Mkuu na zilizobaki alipewa na wageni walioshiriki hafla hiyo.

Waziri Mkuu pia aliwapatia washindi wa pili na wa tatu sh. 15,000 na sh. 10,000/- kila mmoja.