MKE
wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda amesema kila mtu hana budi kumshukuru Mungu kwa
kumfikisha salama wakati wa sikukuu ya Noeli kwani kuna wengine ambao
walitamani kuiona siku hii lakini wameshindwa.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Desemba 25, 2012) wakati wa ibada ya Krismasi
iliyofanyika katika kigango cha Kibaoni kata ya Kibaoni wilayani Mlele, mkoani
Katavi.
“Tunapaswa
kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika sikukuu hii, mpaka leo ni mapenzi yake
hakuna binadamu ambaye ana amri na maisha yake. Tutakumbuka hata mwaka jana
tulikuwa na Askofu wetu wa Jimbo la Mpanda lakini leo hii hatunaye, hivyo sote
tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai,” alisema.
Alisema katika kuadhimisha sikukuu
hii watu hawana budi kuwa na kiasi, wasinywe sana hadi kusababisha magomvi. Aliwasihi
wazazi wawe karibu na familia zao, na wawajibike kwao.
”Tumuombe Mungu atupe neema, yale
tuliyokosea mwaka 2012 tuyaache, tujiandae kuingia mwaka 2013 na yale mazuri
tuliyoyaona mwaka 2012,” alisema.
Naye Padre John Giji wa Shirika la
Wamisionari wa Mt. Thomas ambaye aliongoza ibada hiyo, aliwataka waumini wa kigango
hicho kuwajali wenye shida na siyo kujiingiza katika matendo mabaya wakati wa
sikukuu.
“Kuishi
kwetu kuanzia leo lazima kuwe na mabadiliko, ni lazima tuwajali wenzetu katika
shida zao kwani kwa kufanya hivyo, tutakuwa na mabadiliko ya kiroho na hivyo
kuweza kukua kiimani,” alisema Padre John ambaye pia ni Paroko wa Usevya.
“Wako
watu wanasherehekea Krismasi kwa matendo mabaya kama vile uzinzi na ujambazi. Huo siyo
ukristu tunaotegemewa kuwa nao katika familia takatifu ya Mungu. Tukifanya kazi
kwa bidii, hatuwezi kuwa na tamaa ya vitu vya wengine,” alionya.
“Leo ni sikukuu, tufurahi kwa amani
bila jazba za kidunia. Tusherehekee kwa upendo na amani, ” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment