Makubaliano yameafikiwa kuondoa
kizuizi cha kusafirisha mafuta mashariki mwa Libya. Mauzo ya mafuta
katika nchi za ngambo nchini humo yaliathirika pakubwa katika kipindi
cha miezi minane iliyopita baada ya kufungwa kwa bandari zilizo katika
eneo la mashariki linalotawaliwa na makundi ya wanamgambo.
Katika mkutano wa waandishi wa habari
uliofanyiwa katika jiji la Beghazi, Waziri wa Maswala ya Haki wa Libya,
Salah Al-Maghani, alithibitisha kuondolewa kwa muda kwa vizuizi vya
kuuza mafuta.
Vituo vya mafuta vya Hureiga na
Zuetina vilivyo na uwezo wa kuzalisha mafuta mapipa 200,000 kwa siku
hivi sasa vimesimamiwa na Serikali.
Vituo viwili vilivyo vikubwa zaidi nchini humo
vya Mashariki mwa nchi vya Ras Lanuf na Sidra vitafunguliwa kwa muda wa
majuma machache yajayo, kulingana na Waziri.
Mapatano yaliafikiwa kati ya makundi ya
wapiganaji yaliyosababisha kufungwa kwa vituo hivyo na kundi ambalo
Serikali ililitaja kama "wapatanishi". Msemaji wa Waziri Mkuu ameambia
BBC kuwa Serikali imekubali kuwalipa mishahara walinzi wa vituo hivyo
vya mafuta.
Juhudi za mwezi uliopita za kufikia mapatano ya kuanza kuuza mafuta tena katika vituo hivyo hazikufaulu.
Wale wanaozuia mafuta kuuzwa katika vituo hivyo
wamekuwa wakilalamika kuwa sekta ya mafuta nchini Libya inakabiliwa na
ufisadi mkubwa, lawama ambayo imekanushwa na maafisa wa Serikali.
Wapiganaji hao pia wamekuwa wakisema kuwa wakaazi wa Mashariki
wanahitaji mapato makubwa zaidi kutoka kwa mauzo ya mafuta. Waziri wa
Haki sasa anasema kuwa Serikali itachunguza lawama za ufisadi.
Libya imepata hasara ya zaidi ya Dola Bilioni
tisa tangu kufungwa kwa vituo hivyo vya mafuta. Eneo la Mashariki ndilo
linalozalisha kiwango kikubwa cha mafuta.
BBC
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment