Wiki ngumu CCM 
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Jakaya Mrisho Kikwete
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaanza wiki ngumu ya kusaka theluthi mbili ya kura za wajumbe kutoka Zanzibar ili kiweze kubatilisha mapendekezo ya rasimu ya Katiba ya muundo wa muungano wa serikali tatu.
 
Chama hicho kinachotetea muundo wa serikali mbili, kimekuwa katika harakati za hapa na pale kutafuta uungwaji mkono wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wenye msimamo tofauti.

Wajumbe wa Bunge hilo kupitia kamati zao kumi zenye wajumbe kati ya 52 na 53, kesho wanaanza kuijadili rasimu kwa kuchukua sura ya kwanza na ya sita.

Sura hizi ni nyeti, kwa sababu ndizo zitatoa mwelekeo wa ama muungano utabaki kuwa wa serikali mbili kama CCM inavyotaka au serikali tatu zilizopendekezwa na wananchi kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Sura ya kwanza ya rasimu imegawanywa katika sehemu mbili, ambapo sehemu ya kwanza inazungumzia jina, mipaka, alama, lugha na tunu za taifa.

Sehemu ya pili ya sura hiyo, inazungumzia mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya Katiba.

Sura ya sita inahusu muundo wa Jamhuri ya Muungano. Mambo yaliyowekwa ni muundo wa muungano, vyombo vya utendaji vya Jamhuri ya Muungano, mamlaka ya Serikali ya Muungano, mambo ya muungano na nchi washirika.

Yapo pia mamlaka ya nchi washirika, uhusiano kati ya nchi washirika, mawaziri wakaazi, mamlaka ya wananchi na wajibu wa kulinda muungano.

Katika taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyotolewa na Jaji Joseph  Warioba, wakati akiwasilisha rasimu ya katiba bungeni, alisema kuwa waasisi wa taifa waliacha muungano wa nchi moja, serikali mbili lakini sasa kuna nchi mbili serikali mbili.

Warioba alisema kuwa muungano umefikia hapo kutokana na kile kilichoitwa mchafuko wa kisiasa visiwani Zanzibar mwaka 1984 na hatimaye kuzaa mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar, ambayo yanakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Kwa mantiki hiyo, Jaji Warioba alisema muundo wa serikali mbili hautekelezeki tena kutokana na viongozi kushindwa kusimamia azimio la kutoka serikali mbili kuelekea serikali moja.

Mapendekezo hayo ya tume ya Jaji Warioba yameivuruga CCM, hivyo kutumia kila aina ya mbinu kuhakikisha serikali tatu hazipiti katika Bunge Maalumu la Katiba.

Mbinu zilizofanywa tangu Warioba awasilishe rasimu hiyo ni kumtumia Rais Jakaya Kikwete, kuiponda tume hiyo akidai takwimu zao kuhusu idadi ya watu waliotoa maoni juu ya muundo wa muungao hazina mashiko.

Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya rasimu kama wakiamua kuendelea na serikali mbili mambo mengi yatatekelezeka lakini kwa serikali tatu hayawezekani.

Alisema kuwa serikali tatu hazitekelezeki kwa sababu rais wa shirikisho ana dola isiyokuwa na ardhi na rasilimali za kiuchumi, hivyo serikali yake haiwezi kukopesheka.

Katika kupigia debe serikali mbili, rais aliwatisha wajumbe wa Bunge la Katiba akisema muundo wa serikali tatu ulivyo iko siku jeshi linaweza kupindua serikali za washirika, kupiga na kufukuza watu kisha wakavua magwanda na kuingia madarakani.

CCM katika kujiimarisha kuhakikisha inahodhi mchakato huo, makada wake wakiwemo mawaziri ndio wamechaguliwa kuongoza kamati 12 za Bunge hilo kati ya 14 ambazo wenyeviti wake ndio wanaunda kamati ya uongozi.

Pia chama hicho kimefanikiwa kutumia wingi wake kuamua wajumbe wa Bunge hilo watumie kura mseto (wazi au siri) wakati wa kupitisha ibara na sura za rasimu kwa kuhofia kusalitiwa na wajumbe wake.

Hata hivyo, juhudi hizo ni sawa na kazi bure endapo CCM itakosa uungwaji mkono wa idadi ya theluthi mbili ya wajumbe kwa pande zote mbili za Bara na Visiwani.

Pamoja na kudhibiti mfumo wa upigaji kura uwe wa mseto, sura ya sita kuhusu muundo wa muungano CCM haitaweza kuwabana wajumbe kutoka Zanzibar kwani wengi wao wanataka serikali tatu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa walitarajia kuona CCM ikijenga ushirikiano na CUF kwa upande wa Zanzibar kutokana na wote kuwa katika serikali ya umoja wa kitaifa ili kutumia kura zake chache na zile za washirika kupata idadi inayotakiwa lakini haikuwezekana.

Kwa mujibu wa sheria iliyounda Bunge Maalumu la Katiba, ili uamuzi wowote uweze kufikiwa wakati wa kupitisha ibara au sura kwenye kamati na Bunge, sharti kuwe na theluthi mbili ya kura kwa pande zote.
CCM katika kujirahisishia njia, ilijaribu kutumia wajumbe kupitia kamati ya uongozi kuleta mapendekezo ya marekebisho ya kanuni kadhaa za Bunge hilo ikiwemo kanuni ya 64(1).

Katika mapendekezo hayo ambayo yalikataliwa na wapinzani, kamati ilitaka kurekebisha hanuni hiyo ya 64(1) kwa kuondoa sharti la uamuzi wowote kwenye kamati kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.

Badala yake ilipendekezwa kwamba mwenyekiti wa kamati atawahoji wajumbe ambapo walio wengi watashinda. Hapa ndipo CCM imegonga kisiki kingine katika harakati zake za kutetea serikali mbili.

Mjumbe wa Bunge la Katiba, John Mnyika, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa CCM ilishikilia msimamo wa upigaji kura mseto ikiamini kwamba watautumia kutekeleza azima yao kuhusu waraka wao wa siri na maelekezo ya hotuba ya Mwenyekiti wao, Kikwete.

“Matokeo ya juzi yatatusaidia kujipanga kudhibiti mbinu zao za kuhujumu rasimu ya Warioba kinyume cha maoni ya wananchi na uchambuzi wa wataalamu.

“Hata hivyo, kura hizo hazitoi picha kamili ya kura zitakavyokuwa kwenye sura ya kwanza na ya pili, kwa kuwa; kura za juzi zilikuwa juu ya utaratibu wa kura,” alisema.

Kwa mujibu wa Mnyika, wapo wajumbe waliokubaliana tu na utaratibu ili Bunge lisonge mbele lakini likija suala la muungano, watapiga kura tofauti.

Aliongeza kuwa kura juzi ilikuwa ya wajumbe kwa pamoja wakati kura kuhusu rasimu kila upande wa muungano utapiga tofauti na kura hazitahesabiwa kwa wingi wa kawaida bali theluthi mbili ya kila upande wa muungano na CCM haina theluthi mbili Zanzibar.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top