Kingunge Ngombale Mwiru
Akiwa msemaji wa mwisho katika semina maalum ya kupata uzoefu wa michakato ya katiba, mzee wetu huyu (namheshimu sana) aliibua vifijo, nderemo na hoihoi pale alipomhoji mwanasheria mkuu mstaafu wa Kenya na Seneta wa sasa Busia Mhe. Amos Wako kuhusu umuhimu wa katiba katika kukuza uchumi wa Afrika.

Mzee Kingunge alieleza kuwa haya MAKATIBA kibao yana "role" gani katika kuinua uchumi wa nchi husika, akitolea mfano wa nchi kama Vietnam, Malaysia, Singapore n.k ambazo ziliwahi kuwa sawa kiuchumi na Tanzania lakini leo wenzetu wako mbali mno. Mzee wetu anahoji baada ya miaka hamsini nchi zetu hizi ni masikini sana. 

Mzee Kingunge anasema hata Rasimu ya Katiba ya Jaji ya Warioba ya juzi imejaa masuala ya mitandao ya uongozi na kugawana madaraka tu, anasema hakuna kipengele kinachoelekeza uchumi wa nchi zetu uendeje, usimamiweje, baada ya miaka hamsini uwe wapi n.k.

Anahoji uzoefu wa mwanasheria Amos Wako katika katiba hizi!
Amos Wako amemjibu kwa kifupi, kwamba Katiba ni msingi mkubwa sana wa kujenga uchumi Imara, lakini pia amemkumbusha kuwa kupitisha katiba ni jambo moja, na kuilinda, kuifuata na kuitekeleza ni jambo lingine. Amesisitiza kuwa katiba lazima ifuatwe, na viongozi na wananchi wote wahakikishe inafuatwa vinginevyo haitakuza uchumi.

Kwa mtizamo wangu, Amos Wako amesahau jambo moja muhimu, kwamba uchumi wa nchi nyingi za Afrika unakuwa duni mno kwa sababu viongozi wenye dhamana, marafiki zao na ndugu zao na wanamtandao wao wanatenda na kufanya kila wawezalo kukwapua kila faida inayotokana na jasho la wananchi na kujaza matumbo ya mitandao yao.

Leo pana viongozi kibao wana mabilioni ya fedha katika akaunti za nje. Wazee wetu kama kina Andrew Chenge (Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Tanzania) alipata mgao wa dola milioni mbili katika kashfa ya ununuzi wa rada ya bei kubwa kupita mfano, alipoulizwa kuhusu mapesa hayo(sawa na milioni elfu mbili za Tanzania) alijibu kuwa hivyo ni Vijisenti tu.

Mzee Kingunge mwenyewe anayehoji ati kwa nini nchi za Afrika Kiuchumi zinazidi kuwa hoi, ni juzi tu kwa miaka kadhaa kampuni yake ilikuwa na kashfa kubwa ya kukusanya ushuru stendi ya mkoa bila kutoa gawiwo la haki na linalostahili kwa serikali. 

Tathmini ilionesha kuwa, karibu fedha zote ambazo kampuni yake inakusanya zinalimbikizwa kwa faida ya kampuni. Hata tenda yenyewe ya kutoza ushuru aliipata kwa njia zisizo halali na palikuwa na mvutano mkubwa sana juu ya uhalali wa kampuni hiyo kukusanya ushuru ambao haieleweki hadi leo ulikuwa unakwenda wapi. Kwa kiasi kikubwa kupewa tenda ile kulihusishwa na yeye kuwa karibu na mfumo wa serikali.

Leo Kingunge yuleyule anahoji kwa nini nchi zetu ni masikini mno. Hakumbuki kampuni yake ilitafuna fedha ngapi ambazo wananchi walilipa ushuru Ubungo stendi na anasahau kuwa ikiwa jambo hilo lingetendwa kwa haki fedha zile zingeweza kurudi na kujenga barabara, shule, maji safi, madawa hospitalini, pembejeo kwa wakulima n.k.

Mzee wetu Kingunge anasahau kuwa fefha hizo ambazo kampuni yake ilizitia kapuni zingeweza kabisa kutosha kuondoa sehemu ya umasikini mkubwa unaoikabili nchi yetu. Kwa bahati mbaya sana, baada ya
miaka hamsini ya uhuru ambao yeye alikuwa sehemu yake na miaka hamsini ya uongozi wa CCM ambapo naye amekuwa kiongozi, miaka hiyo yote imepita na kuisha, na leo ndiyo Mzee wetu anakuja kumuuliza kijana mdogo tu kama Amis Wako, amsaidie kujibu swali la WHY AFRICA IS POORER DESPITE THE PRESENCE OF MAKATIBA LUKUKI!

Kwa mtizamo wangu, ni bora Jaji Warioba ambaye amewahi kuwa sehemu ya matatizo ya nchi hii, anapotoka hadharani na kutoa SULUHU ya baadhi ya matatizo hayo, kuliko Mzee Kingunge ambaye amekuwa sehemu ya matatizo kwa miaka hamsini na leo hii bado anatuuliza sisi vijana kwa nini nchi zetu ni masikini.

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru anapaswa kukumbuka kuwa vijana wa sasa tunasoma na tunafanya uchambuzi mkubwa sana, hatuwezi kudanganyika kwa falsafa zisizoeleweka. Ukweli ni kuwa Afrika ina utajiri mkubwa, Tanzania ni tajiri hasa, ila utajiri wote huo unaporwa na kikundi cha watu wachache na wawekezaji bila kuacha faida yoyote kwa mwananchi wa kawaida.

Imefika wakati sasa katiba za Afrika zilinde kwa nguvu zote rasilimali za nchi husika na ziweke utaratibu maalum wa kiuwajibikaji ambapo kila serikali inayokuja madarakani itawajibika moja kwa moja na kwa uwazi, kuhakikisha kuwa rasilimali, nguvu kazi na maliasili za Afrika zinatumika kwa kuwanufaisha wananchi moja kwa moja badala ya kuendelea kuwanenepesha VIONGOZI WACHACHE na mitandao yao.
J. Mtatiro
FB 

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top