Gaudensia: “Kwa hiyo umeacha makusudi ili kunithibitishia kuwa ulikuwa ukitembea na wanawake ovyoovyo?”
Reina: “Siyo kutembea ovyoovyo, kwani wewe ulitegemea muda huo wote
ningekuwa bila mwanamke? Acha utani kabisa, hata wewe kule Dodoma mimi
nitajuaje kama siku zote hukuwa na wanaume? Tena nyie wanafunzi wa Udom
kwa wabunge ndiyo zenu.”
Baada
ya kuzungumza hivyo, Gaudensia alianza kufanya usafi kwa kuchukua
kondomu zote, zile zilizotumika na ambazo hazikuwa zimetumika kisha
akaenda kuzichoma moto. Hata hivyo, maisha hayakuwa na amani kabisa,
vitimbi viliendelea kuchukua nafasi.
Kuna wakati Gaudensia alipigiwa simu na wanawake wa Reina kumtukana
lakini hakuwajibu, alinyamaza na hata mume wake aliporejea nyumbani wala
hakumuuliza. Alichojali yeye ni kujenga ndoa ya yake, aliamini upo
wakati mume wake atabadilika na maisha yatakuwa mazuri.
Uvumilivu wake ulifika ukingoni siku moja baada ya kukuta karatasi
kwenye suruali ya mume wake alipokuwa anafua nguo. Ile karatasi ilikuwa
imeandikwa “WANAWAKE AMBAO NIMESHAWADUU”. Gaudensia akashtuka, akahesabu
majina na kukuta yapo 71.
Gaudensia akagundua kuwa miongoni mwa wanawake hao, wapo marafiki
zake wawili ambao alisoma nao Chuo cha Uhasibu, Kurasini, Dar es Salaam.
Kwenye orodha hiyo kulikuwa na wahudumu wa baa na machangudoa. Ilimuuma
sana.
Reina aliporudi nyumbani, ilikuwa usiku wa manane, kwa hiyo akamuacha
alale, asubuhi alipoamka akamuonesha ile karatasi na kumuuliza sababu
ya kuandika na kuihifadhi. Bila kutarajia, Reina aligeuka mbogo.
Alimkaripia kwa kumchunguza kisha akaanza kumpiga.
Alimpiga na kumuumiza vibaya, baadaye alizimia. Reina bila kujali
kama mkewe hana fahamu, aliita gari na kuchukua kila kitu, aliamua
kuhama nyumba. Hata hivyo, mmoja wa vijana waliokuwa wanabeba vitu,
aliingiwa na huruma, kwa hiyo baada ya kushusha vitu, alikwenda kituo
cha polisi kutoa taarifa.
Polisi walifika pale chumbani na kumkuta Gaudensia bado hana fahamu,
walimbeba mpaka Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mt. Meru ambako alihudumiwa
na kurejewa na fahamu. Polisi wamlitia nguvuni Reina lakini baada ya
Gaudensia kupona, alikana kupigwa na Reina.
Hakutaka mume wake aingie kwenye matatizo. Pamoja na imani hiyo
lakini Reina hakumjali na alimpiga marufuku kufika nyumbani kwake
alipohamia na alikataa kabisa kumuelekeza. Ilimuuma sana Gaudensia,
aliomba japo nauli ya kurudi Dar kwa wazazi wake lakini alinyimwa.
Ilibidi Gaudensia ampigie simu mama yake na alipomsimulia mateso
aliyonayo, haraka sana alimkatia tiketi ya ndege na ile anafika Uwanja
wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, mama yake alimwambia: “Mwanangu ni
sawa kuvumilia lakini umetukosea sana, uvumilivu wako ni kama vile huna
kwenu, kwa nini mwanaume akunyanyase kwa kiwango hicho na wewe uwe
kimya?”
Dunia ina kawaida ya kurejesha majibu haraka, miezi sita baada ya
Gaudensia kutimuliwa na Reina, tayari alikuwa ameshapata kazi nzuri
katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), tayari alishajijenga
sawasawa, akanunua kiwanja akiwa na ndoto za kujenga nyumba ndani ya
miezi 10 inayofuata.
Reina alishafukuzwa kazi wakati huo, mambo yalishaharibika, wazazi
wake hawakutaka kumuona. Mtaani alionekana kama kibaka kwa jinsi
alivyochakaa. Maisha yalimdanganya, akarudi kwa Gaudensia kuomba
msamaha. Itaendelea wiki ijayo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment