RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa azma ya Indonesia ya kuzidisha mashirikiano na Zanzibar katika uimarishaji wa sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu kwa kutoa nafasi za masomo nchini humo kutasaidia kufikia lengo lililowekwa katika sekta hiyo nchini.

 Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa  Indonesia  nchini Tanzania Mbe. Zakaria Anshar, Ikulu mjini Zanzibar.
 
Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Balozi Anshar kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini pamoja na kuwapatia nafasi za masomo vijana wa Kizanzibari.
 
Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makususdi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya juu, hivyo azma ya Indonesia kusaida kuiunga mkono Zanzibar kwa kutoa nafasi za elimu ya juu kutasaidia kwa kiasi kikubwa uimarishaji sekta hiyo.
 
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano huo katika sekta ya elimu utaimarika zaidi kwani wanafunzi kutoka nchini humo nao pia watapata nafasi ya kuja kujifunza Kiswahili hapa Zanzibar pamoja na kuimarisha uhusiano na chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
 
Akizungumza juu ya sekta nyengine ambazo Indonesia imeahidi kutoa mashirikiano yake kwa kuiunga mkono Zanzibar ikiwemo sekta ya afya, utalii, utamaduni, biashara na kilimo  Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo ni jambo la busara.
 
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Dk. Shein alisema kuwa kutokana na nchi hiyo kupata mafanikio katika sekta hiyo hasa katika kilimo cha mpunga, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mashirikiano katika sekta ya kilimo hapa nchini.
 
Kwa upande wa sekta ya biashara, Dk. Shein alisema kuwa Indonesia ina historia kubwa ya kibiashara kati yake na Zanzibar, hivyo hatua hiyo itaimarisha zaidi sekta hiyo hasa biashara ya karafuu. Pia, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na nchi hiyo kuwa na vivutio mbali mbali vya utalii pamoja na uzoefu mkubwa walionao sambamba na tamaduni za nchi mbili hizi kulingana kutaweza kutoa mashirikiano kwa pande mbili hizo kwenye sekta hiyo.
 
Aidha, katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo na kuipongeza Indonesia kwa azma yake ya kuiunga mkono Zanzibar.
 
Nae Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Bwana  Zakaria Anshar, alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake ina inathamni uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na Zanzibar na  kusisitiza kuwa kuwepo kwa Ubalozi wa nchi hiyo hapa Tanzania kutarahisisha zaidi mashirikiano pamoja na uhusiano huo.
 
Mhe. Anshar alisema kuwa  Indonesia imeamua kwa makusudi kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu kwa kutoa nafasi za kujiunga katika vyuo vya elimu ya juu nchini Indonesia pamoja na kushirikiana na vyuo vya hapa nchini.
 
Akieleza mafanikio yaliopatikana kwenye sekta ya kilimo, Balozi huyo alisema kuwa Indonesia imeweza kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo hasa katika kilimo cha mpunga ambapo itakuwa ni fursa ya pekee kutoka utaalamu wake kwa Zanzibar.
 
Kwa upande wa sekta ya biashara, Balozi huyo alieleza kuwa mbali ya biashara ya karafuu, pia, ushirikiano huo utawasaidia wafanyabiashara binafsi kutoka Zanzibar kwenda nchini humo kwa ajili ya kununua bidhaa tofauti na wale wa Indonesia kuja Zanzibar.
 
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na  Balozi wa Denmark anayeshughulikia mashirikiano na maendeleo duniani Mhe. Bibi Charlotte Slente aliyefuatana na Balozi wa  Denmark nchini Tanzania Mhe. Johnny Flento huko Ikulu  mjini Zanzibar na kuzungumza masuala mbali mbali yanayohusu sekta ya afya.
 
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar imejiwekea mikakati maalumu katika kuhakikisha sekta ya afya inaendelea kupata mafanikio makubwa.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa licha ya kuungwa mkono na Washirika mbali mbali wa Maendeleo ikiwemo Denmark, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka kipaumbele zaidi katika uimarishaji wa sekta ya afya.
 
Nae Bi  Charlotte Slente alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Denmark itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa ikizingatia juhudi inazozichukua katika kuimarisha sekta hiyo.
 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top