Rais wa Marekani, Barack Obama.

RAIS wa Marekani, Barack Obama, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi hapa nchini mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani iliyolifikia MTANZANIA Jumapili imeeleza kuwa ziara hiyo ya Rais Obama itajumuisha mataifa manne ya Afrika, ambayo ni Nigeria, Afrika Kusini, Tanzania na Rwanda.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, akiwa nchini Nigeria, Rais Obama atafanya mazungumzo na Rais Goodluck Jonathan pamoja na maofisa wa juu wa Serikali ya nchi hiyo.

Wachambuzi wa mambo wanasema, mazungumzo hayo yamelenga kutafuta njia za kutokomeza makundi ya wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram, ambao wamekuwa wakiendesha videndo vya ugaidi nchini humo.

Kundi la wanamgambo wa Boko Haram, ambalo maskani yake yapo Kaskazini mwa nchi hiyo, limekuwa likifanya vitendo vya kigaidi katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo.

Hata hivyo, taarifa hiyo imeeleza Rais Obama, awali alikuwa na mpango wa kufanya ziara ya siku mbili Nchini Nigeria, lakini kutokana na kuwapo na hali ya wasiwasi wa kiusalama, atatumia saa chache au siku moja katika taifa hilo.

Ziara hiyo ya Obama barani Afrika itakuwa ya mara ya pili, ikitanguliwa na ya mwaka 2009, alipotembelea taifa la Ghana ambako alikutana na Rais John Atta Mills, ambaye sasa ni marehemu na kuhutubia Bunge la Ghana pamoja na kutembelea soko la watumwa waliovushwa Bahari ya Atlantic wakati wa biashara ya utumwa, Ngome ya Pwani ya Cape.

Kutofika kwa Obama nchini Nigeria katika ziara yake awali, kulizua hoja mbalimbali kutoka kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia, ambapo baadhi walieleza uamuzi huo ni kuisusa Serikali hiyo, mtazamo ambao aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, aliukana.

Clinton alisema uchaguzi wa Obama kuanza na Ghana katika ziara yake Afrika ulimaanisha kukuza uhusiano baina ya Marekani na Jangwa la Sahara, Afrika na hivyo uchaguzi huo usitafsiriwe kwa namna nyingine yoyote.

Wakati wa ziara hiyo, masuala yanayotarajiwa kuzungumzwa ni uhusiano wa biashara, usalama na haki za binadamu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top