Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
HATIMAYE Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewatia mbaroni askari 16 wanaohusishwa na tuhuma za uhalifu.

Kutangazwa kwa taarifa hiyo kunakuja siku chache baada ya Tanzania Daima kuandika habari juu ya polisi hao kwa kushirikiana na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuunda mtandao wa kihalifu.

Taarifa ya kukamatwa kwa askari hao zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Kova alisema askari hao wanatuhumiwa kuunda mtandao wa kukusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara wasiotaka kulipa ushuru wa serikali.

Licha ya kuweka wazi idadi hiyo kamanda Kova aligoma kuyataja majina ya wahusika bila kuweka wazi kwa nini ameamua kufanya hivyo.
Kova pia alitumia muda huo kuilaumu Tanzania Daima, kwa kuandika habari za uhalifu huo juzi ikiwa ni baada ya uchunguzi wa zaidi ya wiki moja tangu kukamatwa kwa askari hao.

Alisema kabla ya gazeti hili kuandika habari hizo kwa mara ya kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, jeshi hilo lilikuwa limeshawakamata askari wake wanane kutokana na tukio hilo.

Mei 10, Tanzania Daima ilimuuliza kamanda Kova juu ya habari hizo lakini alikataa kuzitolea ufafanuzi kwa madai angelizungumza na waandishi wengi.

Bila kujali jitihada za Tanzania Daima kuipata habari hiyo kamanda Kova alijinasibu kuwa angelizitoa kwa utaratibu aliojiwekea yeye na wala si kwa kuulizwa na gazeti moja moja.

“Si kwa kuwa gazeti moja liliandika na ndiyo tumesukumwa kuwakamata wahalifu hawa; tulianza taratibu hizi mapema na tukawa tunasubiri muda muafaka wa kuweka mambo yote hadharani,” alisema Kova.

Hata hivyo Kova jana alishindwa kuweka wazi yalikopelekwa magari yaliyokamatwa kwenye uhalifu husika.

Wakati akishindwa kutaja kama kuna magari yaliyokamatwa, baadhi ya askri waliozungumza na gazeti hili wameshangazwa na hatua hiyo na kumtaka DCP Kova awe mkweli juu ya sakata hilo.

Askari hao wamehoji hatua ya Kova kuwakamata wenzao walioonekana katika picha za video za mnato na kushindwa kuyakamata magari yaliyokubali kushiriki katika uhalifu huo.

“Mnapaswa kujiuliza kama askari wameshafika 16 halafu hakuna gari hata moja lililokamatwa, hao watakuwa wanapelekwa mahakamani kwa ushahidi wa namna gani na kwa nini hayo magari hayakuweza kuchukuliwa katika hizo picha au ni siasa za mzee wetu zimewafanya mkashindwa kuhoji hilo?” alisema mmoja wa askari.

Tanzania Daima mwishoni mwa wiki iliandika juu ya kuwepo kwa mtandao unaowashirikisha askari wa vyeo mbalimbali kutoka jijini Dar es Salaam na baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) wakiwa wamejiundia mtandao wa kukusanya pesa kutoka kwa wafanyabiashara wasiotaka kulipa ushuru.

Mtandao huo unadaiwa kufanya kazi kwa takriban miezi sita kabla ya kujulikana na kuchukuliwa kwa hatua dhidi yao.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha Tanzania Daima, mbinu inayodaiwa kutumiwa ni kwa askari hao kuwasaidia wafanyabiashara kuingiza bidhaa kupitia bandari bubu ya Mbweni, kisha kuzipakia kwenye magari makubwa kwa ajili ya kutawanya bidhaa hizo katika masoko ya jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya bidhaa zinazodaiwa kuingizwa kwa wingi ni runinga, redio, pasi za umeme na kompyuta mpakato.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top