Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohammed Mpinga.
JESHI la Polisi jana limeanza kufanya ukaguzi wa leseni na vyeti vya
madereva kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani na nchi jirani Ubungo
(UBT), jijini Dar es Salaam kufuatia ajali za barabarani nchini
kuongezeka.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema kuwa ukaguzi huo una lengo la
kuchunguza madereva ambao wanafanya shughuli hizo kinyume na sheria na
kusababisha kuwapo kwa ajali nyingi za barabarani.
“Lengo letu ni kuhakikisha madereva wanakuwa na vyeti pamoja na
leseni halali. Hakuna atakayeachwa katika zoezi hili kwa sababu
linaendeshwa katika mikoa yote ambayo mabasi makubwa yanasafiri ili
kuepusha ubabaishaji wa madereva,” alisema.
Kuhusu malalamiko ya kuwapo urasimu katika zoezi hilo, Kamanda Mpinga
alisema hata kama dereva hatakaguliwa katika kituo cha Ubungo,
atakwenda kukaguliwa mikoani ili kufanikisha zoezi hilo.
Umoja wa Madereva wa Mabasi (UWAMATA), ulilalamikia kuwapo kwa
urasimu katika zoezi hilo kwa madai kuwa madereva wengi hawajakaguliwa.
Mmoja wa wajumbe wa umoja huo, Jabu Chagenya, alisema serikali
inapaswa kuwa na nia ya dhati katika kupambana na tatizo hilo na kuacha
kutimiza majukumu yake kisiasa.
“Huwezi kufanya ukaguzi wa aina hii kwa kuuliza namba ya leseni
pamoja na kuhoji cheti, ingepaswa kuwapo kwa ushirikishwaji wa Chuo cha
Taifa cha Usafirishaji na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi ili
kutambua vyeti hivyo kama ni feki.
“Kilichotokea ni usumbufu kwa abiria na kama wataendelea kufanya
ukaguzi kwa mtindo huu sidhani kama utakuwa na mafanikio kwa kuwa watu
ambao tunajua matatizo ya madereva hatushirikishwi,” alisema Chagenya.
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment