Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta akitoa maelezo muhimu
wakati wa mjadala wa Bunge hilo leo 10 Septemba, 2014 Bungeni mjini
Dodoma.
Baadhi
ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa ndani ya Bunge hilo leo
10 Septemba, 2014 kwa ajili ya kuendelea na mjadala wa Rasimu ya Katiba.
………………………………………………………
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
BUNGE
Maalum la Katiba leo tarehe 10 Septemba, 2014 limeendelea na kazi yake
ya kusoma na kujadili taarifa za Kamati mbalimbali Bungeni mjini Dodoma.
Baadhi
ya mambo yaliyojadiliwa katika Bunge hilo ni pamoja masuala ya migogoro
ya ardhi inayowahusisha wafugaji na wakulima, mambo ya Uraia pacha,
haki ya afya, haki ya kuishi ikiwemo sheria ya kunyonga, haki za
binadamu, haki ya Mtuhumiwa na Mfungwa, haki za wafanyakazi na ajira
pamoja umri katika ajira pamoja haki za vijana.
Akizungumza
wakati wa mjadala huo, Mjumbe wa Kamati namba Sita, Mhe. Zaina Madabida
amesema kuwa ni vema kuwepo kwa kipengele kinachotambua mila na desturi
za makundi ya wafugaji na wakulima ili kuondoa migogoro ya ardhi ambayo
imekuwa ikijitokeza mara kwa mara hapa nchini.
Kuhusu
masuala ya Uraia, Mhe. Madabida ameeleza kuwa si vema kumtambua mtoto
mwenye miaka Saba kama raia Mtanzania aliyekanyaga katika ardhi ya
Tanzania na badala yake ni vema mtoto mchanga ndiyo atambulike kama raia
halisi wa Tanzania kikatiba kama Mtanzania, hivyo yeye na Kamati yake
wamekubaliana kumtambua mtoto mchanga kama Mtanzania halisi ambaye
atakuwa amekanyaga katika ardhi ya hiyo.
“Mtoto
ambaye ni raia halisi wa Tanzania atakayekutwa katika ardhi ya Tanzania
itambulike kuwa ni yule mtoto mchanga na sio yule mwenye umri wa miaka
Saba”, alisema Mhe. Madabida.
Aidha,
Mhe. Madabida amegusia suala la Sheria ya Haki ya kuishi pamoja na
Sheria ya kunyonga akisema kuwa Sheria hiyo ya kunyonga ni vema iendelee
kuwepo katika Katiba kwani kuna watu ambao wao wanaua wenzao.
“Adhabu
ya kifo iendelee kuwepo kama Katiba yetu ya sasa inavyosema kwani kuna
watu wao wamekuwa wakiwaua wenzao”, alisema Mhe. Madabida.
Kwa
upande mwingine, mjumbe toka kamati namba Tisa amezungumzia kuhusu
suala la haki za binadamu akitaja Ibara ya 24 katika Sura ya Nne, nae
amesema kuwa maoni ya wachache yamefafanua kuwa haki ya kuishi ianzie
tangu pale mimba inapotungwa kwani sikuhizi watu wengi wamekuwa na
utaalamu sana katika kutambua viumbe vilivyopo tumboni, hivyo watu hao
wamekuwa wakikatiza uhai wa viumbe wasiokuwa na hatia.
Mjumbe
ameongeza kuwa katika Ibara ya 39 inayohusu haki ya Mtuhumiwa na
Mfungwa, yeye na kamati yake wameitaka Katiba izingatie mazingira rafiki
kwa watuhumiwa wenye ulemavu na izingatie kuhusu suala la miundombinu
kwa walemavu hao ili iwe rafiki kwani Magereza mengi nchini yalijengwa
kipindi kirefu.
Naye
mjumbe wa kamati namba Kumi, Mhe. Monica Sophu amezungumzia kuhusu
suala la ardhi akisema kuwa katika mambo yanayohusiana na masuala ya
ardhi, ni vema ikaundwa Tume Huru ya Ardhi ambayo itakuwa ina kazi ya
kushughulikia masuala hayo ili kuepusha migogoro inayojitokeza baina ya
makundi mbalimbali.
“Katika
kutatua suala la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, ni
vema kukawepo na Tume Huru ya Ardhi itakayoshughulikia masuala hayo,
hivyo Katiba iwatendee haki makundi haya”, alisema Mhe. Sophu.
Naye
mjumbe wa Kundi la 201, Mhe. Jesca Msavatavangu amezungumzia juu ya
haki za Vijana nchini akisema kuwa, haki hizo za vijana hazijaainishwa
vema, hivyo ameshauri kuwa ni vema sasa Katiba ikaainisha vema haki hizo
ikiwemo kuelezea juu ya ushiriki wao katika nafasi za uongozi pamoja na
kupewa fursa kushiriki katika mambo ya kiuchumi.
“Serikali
iweke namna ya kuwaelimisha vijana wetu kuhusu kazi ili wawe na ujasiri
na wajengewe uwezo, pia vijana wapewe fursa ili waweze kushiriki katika
nyanja za kiutamaduni, walindwe dhidi ya afya na uhai wao”, alisema
Mhe. Msavatavangu.
Kuhusiana
na suala la Uraia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Msavatavangu
amesema kuwa Sura ya 56 inayohusu suala la uraia huo ni vema
likachukuliwa kwa umakini mkubwa, aidha ameshauri kuwa ni vema kuwa na
uraia wa nchi moja kwani Tanzania bado haijaweza kujilinda vyakutosha
kuweza kukabiliana vitendo viovu vinavyoweza kujitokeza.
“Watu
watatumia fursa hii ya Uraia pacha kuhujumu uchumi wetu, kwani kuna
mazingira mengi ya rushwa, hivyo suala la hili la uraia pacha lije
kufikiriwa baadaye sana sio sasahivi”, alisema Mhe. Msavatavangu.
Naye
mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Mhe. Yahya Kassim Issa amegusia kuhusu
suala hilo hilo la Uraia pacha akitaja Ibara ya 38 inayohusu suala la
uraia, amesema kuwa kuna watu wenye watoto wao nje ya nchi na kwa
ubinafsi wao ndiyo wanatumia nafasi hiyo kudai uraia huo badala ya
kujali uzalendo na usalama wa nchi yao.
“Haiwezekani kwa mtu uwe na uraia wa nchi mbili halafu uwe Mwadilifu katika nchi zote hizo mbili”, alisema Mhe. Issa.
Bunge
hilo linaendelea na kazi ya kusoma na kujadili taarifa za kamati
mbalimbali kama ilivyopangwa ambapo wajumbe toka kamati husika
wanachangia michango toka katika kamati zao kwa lengo la kujadili ndani
ya Bunge hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment