Moto wa Msigwa wazindua serikali 
 Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa
SIKU chache baada ya Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa kuonyesha video ya jinsi Kampuni ya uwindaji ya Green Miles Safaris Ltd, inavyokiuka sheria za uwindaji kwa kutesa wanyamapori, serikali imezinduka usingizini na kuchukua hatua za kuifutia umiliki wa vitalu vyake vyote.

Julai 4 mwaka huu, Mchungaji Msigwa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alionyesha ushahidi wa video aliyoiwasilisha katika kikao cha Bunge la Bajeti mwaka 2014/15, akidai kampuni hiyo imekuwa ikifanya vitendo vinavyokiuka sheria ya mwaka 2009 ya uhifadhi, ambayo inatumika pamoja na Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 na kutaka serikali ichukue hatua.

Akifafanua tuhuma hizo jana kwa waandishi wa habari, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema kuwa baada ya Msigwa kuwasilisha ushahidi huo, aliagiza Idara ya Wanyamapori ifanye uchunguzi wa kina kubaini ukweli dhidi ya tuhuma husika, ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya kampuni iliyotuhumiwa.

“Tuhuma hizi zinatokana na Kampuni ya Green Miles Safaris Ltd kufanya uwindaji katika kitalu cha Gonabis/Kidunda- WMA na kitalu cha MKI- Selous, katika kipindi cha uwindaji cha mwaka 2012.

“Aidha, baada ya kusikia maelezo yaliyowasilishwa dhidi ya tuhuma hizo, na baada ya timu ya wataalamu wa Idara ya Wanyamapori kupitia video kwa kina, ilibainika kuwa Kampuni ya Green Miles Safaris Ltd ilivunja sheria ya kuhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009,” alisema.

Nyalandu alitaja makosa hayo kuwa ni wageni wa kampuni hiyo kuwinda wanyama ambao hawakuruhusiwa kwenye leseni ya uwindaji wakiwemo nyani na ndege, jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 19(1)(2).

Pili, wageni wa kampuni hiyo kuchezea watoto wa pundamilia na ngiri kinyume na kifungu cha (19)(1), wageni kufukuza wanyamapori kwa magari na kisha kuwapiga risasi wakiwa ndani ya magari kinyume na kifungu 65(1) (a) 1, kuwinda wanyama walio chini ya umri (watoto), kinyume na kifungu cha 56(1).

“Kuruhusu watoto chini ya miaka 16 kuwinda kinyume na kifungu cha 43(2) (a), na wageni kuwinda huku wakipiga kelele, jambo ambalo ni kero kwa wanyama na kinyume na kifungu cha 19(1) na (2),” alisema.

Nyalandu alikiri kampuni hiyo kuvunja sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009, sambamba na kanuni za uwindaji, na kwamba kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa chini ya sheria hiyo ya kuhifadhi wanyamapori No.5, amechukua hatua.

“Kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 17(1), 8(2), nafuta umiliki wa vitalu vyote vilivyo chini ya Kampuni ya Green Miles Safaris Ltd, hii ikiwa ni pamoja na vitalu vya Lake Natron GC East, Gonabis/ Kidunda-WMA na MKI-Selous.

“Pia, hatua hii inafuta vibali vyote vya uwindaji vilivyotolewa katika msimu huu wa uwindaji na hii iwe onyo kwa kampuni za uwindaji wa kitalii nchini kuhusu ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uwindaji,” alisema.

Alipoulizwa watendaji wa idara husika walikuwa wapi wakati ukiukwaji huo ukifanywa na kama hatua hiyo ya kufuta vitalu inakidhi haja, Nyalandu alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu, wageni wa kampuni hiyo walipaswa kuingia kwenye maeneo husika wakiwa na waangalizi wa Idara ya Wanyamapori, jambo ambalo halikufanyika.

Kuhusu adhabu hiyo, alisema kuwa haikidhi haja vya kutosha, lakini akasisitiza kuwa kwa vile ni mara ya kwanza tendo kama hilo kufanyika nchini, serikali itaendelea kuifanyia marekebisho sheria ya wanyamapori ikiwa ni pamoja na kuifumua Idara husika kwa kuiundia bodi.

Alipoulizwa serikali inajipangaje kuhakikisha wahusika hawafanyi udanganyifu wa kuanzisha kampuni nyingine za uwindaji nchini baada ya kufutwa, Nyalandu alisema: “Tutahakikisha tunawaweka kwenye ‘black list’ ili popote watakapojitokeza watambulike kuwa hawatakiwi.”
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top