Nape Nnauye
Siku moja baada ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza kusimamisha mgombea mmoja katika
nafasi ya urais na ubunge majimboni, CCM kimebeza hatua hiyo kikisema
viongozi hao hawawezi kukaa zizi moja.
Akizungumza jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema viongozi wa Ukawa
ni genge la wasaka madaraka hivyo hawawezi kuungana kwa hilo.
Nnauye alisema viongozi wa vyama vya upinzani
waliungana kwa lengo la kutafuta Katiba bora, lakini wamebadilisha
ajenda na sasa wanazungumzia urais mwaka 2015.
“Hawa kumbe ni waongo, malengo yao siyo Katiba,
bali ni kutafuta madaraka, muungano wa kutafuta madaraka hauwezi
kufanikiwa kwa sababu viongozi wote wa Ukawa ni wapenda madaraka,”
alisema Nnauye.
Alisema wananchi watashuhudia umoja huo ukisambaratika kwa sababu viongozi wa Ukawa hawawezi kuvumiliana na kuachiana madaraka.
“Kuungana ni jambo zuri, lakini sababu za kuungana
zinapotajwa kuwa ni kumsimamisha mgombea mmoja wa urais mwaka 2015,
watasambaratika kabla ya muda huo kufika,” alisema.
Alisema Ukawa wamewadanganya wananchi kwamba wanasimamia Katiba bora kumbe ajenda kuu ni kuongoza nchi.
Gazeti hili jana liliripoti kuwa Ukawa pia wanataka kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge katika kila jimbo la uchaguzi.
Katika habari hiyo, Mwenyekiti wa Chadema ambaye
pia ni Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR
Mageuzi, James Mbatia walikiri kuwapo mpango huo.
Taarifa za kuwapo mpango, zimekuja siku chache
tangu kufichuliwa kwa mpango mwingine wa kuundwa upya kwa Baraza la
Mawaziri Kivuli ambalo litawajumuisha wabunge wa vyama vya upinzani
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa bajeti
unaoanza Mei 6, mwaka huu.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment