
HATIMAYE serikali imeweka hadharani kwamba kila mjumbe katika Bunge la Katiba ataweka kibindoni posho ya sh 300,000 kwa siku.
Kwa maana hiyo, kila mjumbe katika Bunge hilo atakuwa amelipwa sh
milioni 21 kwa siku 70 za uhai wa Bunge hilo, na kama serikali itaongeza
siku 20 zaidi kwa mujibu wa katiba na kufikia siku 90, kila mjumbe
atavuna sh milioni 27.
Awali gazeti hili liliwahi kuripoti majadiliano ya ndani serikalini
kabla ya jana kuthibitishwa rasmi ambapo kulikuwa na pendekezo la kutaka
kila mjumbe alipwe sh 700,000 kwa siku.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Katibu wa Bunge
Dk. Thomas Kashililah, alisema kuwa kila mjumbe katika Bunge hilo
atalipwa sh 300,000 kwa siku.
Alisema malipo ya wajumbe hao ni pamoja na posho zote za vikao ikiwa imeunganishwa na posho za madereva.
Pia alieleza kuwa gharama zote ambazo zimetumika katika matengenezo
ya ukumbi na sehemu nyingine ni sh bilioni 8.2 na fedha hizo ni bajeti
ya kawaida ambayo ilipitishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14.
Mbali na hilo, Kashililah alisema kuwa kutokana na umuhimu wa kuwepo
kwa Bunge Maalumu la Katiba, Bunge limehakikisha linafanya ukarabati
ikiwa ni pamoja na kufunga mitambo mbalimbali ya usalama na kurekebisha
mifumo ya kiutendaji.
Alisema matengenezo yaliyofanyika ni pamoja na kurekebisha paa la
jengo la ukumbi wa Bunge ambalo awali lilikuwa likivuja wakati wa mvua.
Akitoa ufafanuzi zaidi katika ufungaji wa viti ndani ya ukumbi wa
Bunge hilo, alisema kuna viti 678 na kurekebisha vipaza sauti ambapo
kazi hiyo pekee imegharimu dola za Kimarekani milioni moja.
Kuhusu maandalizi, alisema yamekamilika na wajumbe wameishaanza kufika bungeni kwa ajili ya usajili.
Alisema vikao vya Bunge vitaanza rasmi Februari 18 majira ya saa
nane mchana na wataanza kwa kumchagua mwenyekiti na makanu wake.
Alisema ratiba ya Bunge la Katiba itaanza na mkutano wa maelekezo kwa
wajumbe Februari 18 asubuhi na Bunge lenyewe litaanza siku hiyo hiyo
saa nane mchana.
Kwa mujibu wa katibu huyo, shughuli nyingine zitakazofanyika ni
pamoja na mwenyekiti wa muda kusimamia uandaaji na upitishwaji wa
kanuni.
Alisema mwenyekiti wa muda atasimamia uchaguzi wa mwenyekiti na baada
ya kupatikana mwenyekiti na makamu wake, ndipo atakapopatikana katibu
ambao wataapishwa na Rais Jakaya Kikwete.
Uhai wa Bunge hilo utakoma Aprili 30 au kwa ridhaa ya rais.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment