Mtoto wa Rais wa zamani wa Zambia, Andrew Banda amehukumiwa
kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kutiwa hatiani katika makosa ya
kuhusika na rushwa.
Andrew (53), mtoto wa aliyekuwa Rais Rupiah Banda
pia aliwahi kuwa mwanadiplomasia, alikamatwa mwaka 2012 akidaiwa kupokea
rushwa kutoka kwa Kampuni ya Fratelli Locci ya Italia iliyopewa zabuni
ya ujenzi wa barabara.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Joshua Banda alisema
kwamba amezingatia maelezo yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka kwamba
mtuhumiwa huyo ndiye mhusika mkuu katika kosa hilo la kudai na kupokea
rushwa, lakini ni mara yake ya kwanza kutiwa nguvuni.
Alisema kutokana na hali hiyo, ameona ni vyema
kuangalia namna ya kumpunguzia adhabu na hivyo kumhukumu kifungo cha
miezi 24 jela, lakini pia akipewa haki yake ya msingi ya kukata rufaa.
Mahakama pia ilimtia hatiani kwa kushindwa kueleza
kuhusu namna alivyozipata zaidi ya Dola 63,000 zilizokuwa kwenye
akaunti yake, ambazo zinadhaniwa zilipatikana kwa njia zisizokuwa
halali.
Banda, naibu balozi wa zamani wa nchi hiyo nchini
India na aliyewahi kuwa katibu mkuu wa ubalozi wa Zambia nchini Italia
ni mmoja miongoni mwa maofisa wengi kutoka katika utawala wa baba yake
walioshtakiwa kwa kujihusisha na rushwa baada ya kampeni maalumu ya
kupambana na rushwa inayoongozwa na Rais wa sasa, Michael Sata.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment