
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Dk Hamisi Kigwangalla amesema ili kuondoa mvutano kuhusu muundo
wa Muungano ni lazima yafanyike mambo mawili, ambayo ni kuongeza muda wa
Rais kuwa madarakani au kubadili Katiba katika maeneo yanayohusu Tume
ya Uchaguzi (NEC) pekee.
Akizungumza jijini jana, Dk Kigwangalla ambaye ni
Mbunge wa Nzega (CCM) alisema mambo hayo mawili hayawezi kukwepeka
kwa sababu hata kama Katiba Mpya itapatikana, bado itahitajika kufanya
mabadiliko ya sheria mbalimbali, zoezi ambalo alidai litachukua takriban
miaka miwili.
“Namwomba Rais Jakaya Kikwete aingilie kati.
Atumie mamlaka yake kusitisha mchakato wa Katiba mpaka itakapoundwa Tume
nyingine ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala la muundo wa
Muungano,” alisema na kuongeza;
“Baada ya maoni hayo ipigwe kura maalumu kuhusu
jambo hili ili Watanzania washiriki kikamilifu na upatikane uamuzi
sahihi na unaokubalika na wengi. Si jambo la busara kujadili Rasimu ya
Katiba bila kuwa na suluhu inayokubalika kuhusu muundo wa Muungano.”
Alisema kuwa kitendo cha Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kupendekeza muundo wa
Serikali tatu, utalivuruga Bunge la Katiba iwapo wataibuka wajumbe na
kupinga muundo huo.
Alisema kuwa kama muundo wa Serikali tatu
utapingwa, muundo wowote utakaopitishwa utasababisha kuwekwa vifungu
vipya jambo ambalo litazidi kuleta mkanganyiko katika mchakato mzima wa
Katiba.
“Ndiyo maana nikasema mchakato huu usitishwe kwa
muda ili watu wote tukubaliane juu ya muundo wa muungano tunaoutaka.
Wabunge wa Bunge la Katiba tukiukataa huu muundo wa Serikali tatu kipi
kitatokea?”alihoji.
Dk Kigwangalla alisema Tume hiyo bado haijatoa
majibu katika mambo kadhaa; njia ilizotumia kupendekeza Serikali tatu,
kwa nini walipendekeza mfumo huo na nani atakuwa na mamlaka ya kuandika
Katiba ya Tanganyika.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo wakati tayari Rais
Kikwete ameshateua wajumbe 201 wa Bunge hilo ambalo linaanza Februari 18
mjini Dodoma.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment