
Katiba hii ni ya kihistoria tofauti na zile
zilizotangulia ambazo zimekuwa zikifanyiwa marekebisho bungeni bila
wananchi kujua kinachoendelea kwani hawakushirikishwa kuzitunga.
Hivi karibuni Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya
Katiba (jina limehifadhiwa) aliwahi kuhojiwa na mwandishi wa makala haya
kuhusu matarajio ya Watanzania kuhusu Katiba Mpya na matumizi ya
Kiswahili.
Naye alisema: “Nawataka wajumbe wa Bunge la Katiba
watakaokwenda Dodoma kutumia lugha sahihi inayoeleweka kwa wananchi,
badala ya kuchanganya lugha. Wajumbe wasichanganye lugha ‘Kiswanglish’
kama ilivyotokea katika mikutano mingine ya kitaifa hata bungeni.
Hali hii inajitokeza sana siku hizi katika vikao
mbalimbali vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kiswahili ndiyo
lugha rasmi ya Bunge hilo lijalo na tungependa wabunge wazingatie hilo,
maana tunaona baadhi ya mawaziri na wajumbe wengine wakichanganya
lugha.”
Kauli aliyoitoa mjumbe huyu ni ya kupigiwa mfano
kwani ametoa ya rohoni. Ni mzalendo kwelikweli, kwani ameweka mbele
masilahi ya Watanzania wote. Hawa wajumbe wanawawakilisha Watanzania 45
milioni, ambao wana haki ya kujua hatima ya nchi yao kwani
yatakayoamriwa katika Bunge hilo la Katiba yatamgusa kila mwananchi.
Katiba hii ni ya kihistoria tofauti na zile
zilizotangulia ambazo zimekuwa zikifanyiwa marekebisho bungeni bila
wananchi kujua kinachoendelea kwani hawakushirikishwa kuzitunga.
Matumizi ya lugha fasaha na sanifu ya Kiswahili
wakati wa mijadala ya Bunge la Katiba ni jukunu la kila mjumbe. Kwa wale
wenye matatizo kidogo kwa maana ya wasomi walioathiriwa na lugha za
kigeni wajitahidi kujiandaa zaidi kabla ya kuzungumza. Wajitayarishe kwa
kutumia kumbukumbu za kuwaelekeza ni nini cha kuzungumza, wakitumia
mwongozo uliowekwa. Wenzetu wasomi wanatumia maneno ‘talking notes’ kama
kiongozi cha mazungumzo.
Maandalizi ya aina hii yatawawezesha wajumbe
kutumia lugha ya Kiswahili bila hofu, akiamini kuwa wasikilizaji
watafaidika na hoja zake.
Mjumbe huyu wa Bunge Maalumu la Katiba ametoa rai
ya kuachana na tabia ya kuchanganya lugha katika mazungumzo ambayo
imeshamiri kwa Watanzania, wasomi walio wengi.
Hili ni suala lililoguswa na wengi kwamba wabunge
wakiwamo mawaziri huchanganya maneno na hata vifungu vya maneno ya
kigeni wanapochangia hoja bungeni.
Inawezekana wanafanya hivyo kwa
kukosa maneno ya Kiswahili yanayofaa, lakini wanakera zaidi
wanapozungumza. Kwa mfano anaweza kusema;
“Wananchi wa jimbo langu hawana ‘idea’ ya mradi huu wa umwagiliaji ambao ‘donors’ wametoa zaidi nusu ya fedha zote.”
Wako baadhi ya wasikilizaji wataelewa kilichotamkwa bungeni, lakini kwa jumla ni makosa kutumia maneno kama ‘idea’ na ‘donors’.
Kwa utafiti wangu mdogo nimegundua kuwa hatakuwapo Mjumbe wa Bunge la Katiba mwenye elimu chini ya kidato cha nne.
Hiki ni kidato ambacho Kiswahili kilifundishwa kama somo,
kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, baada ya kumaliza darasa la
kwanza hadi la saba kwa shule za msingi ambapo Lugha ya kufundishia ni
Kiswahili.
Iweje wewe Mtanzania uliyepitia mfumo huu wa elimu
yetu uanze kujidai kutumia maneno ya Kiingereza kwenye mazungumzo yako,
tena yaliyo rasmi na ambayo yatahifadhiwa katika mfumo wa kiteknolojia
wa ‘Hansard’.
Namwomba Spika wa Bunge la Katiba ashirikiane na
wajumbe kutunga kanuni za bunge hilo zitakazoweka wazi kuwa lugha ya
majadiliano ni Kiswahili fasaha na sanifu na atakayejaribu kutumia lugha
mseto, atolewe nje, kwani hayuko hapo kwa manufaa ya Watanzania, bali
yake binafsi.
Mwisho, ningetoa ushauri kwa Taasisi ya Taaluma ya
Kiswahili (TATAKI), ambayo imetunga Kamusi ya Kiswahili Sanifu waweke
katika mfumo katika Tovuti, kuonyesha misamiati na istilahi
zilizosanifiwa ili wajumbe wa Bunge la Katiba waweze kupata tafsiri,
maana na matumizi ya maneno ya Kiswahili.
Wajumbe watapata fursa ya kutumia lugha ya
Kiswahili kwa kujiamini na wenzetu watakaokuwa wanafuatilia majadiliano
kutoka katika vyombo vya habari nje ya nchi watakuwa na kumbukumbu za
uhakika kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo.
0 comments:
Post a Comment