Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalumu la Katiba.
 
Kwa ushindi huo, Kificho atakuwa na kazi kuandaa kanuni ambazo zitatumika kwa ajili ya kumchagua mwenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo na kusimamia vikao vyake.
Muda wa mwenyekiti huyo wa muda utamalizika Ijumaa baada ya wajumbe kupitisha kanuni za kuendesha Bunge hilo na kumchagua mwenyekiti na makamu wake.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema Kificho alichaguliwa kwa kura 393 sawa na asilimia 69.13 na kumshinda mpinzani wake Profesa Costa Mahalu aliyepata kura 84 sawa na asilimia 14.79. Kura saba ziliharibika.
Wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Magdalena Rwebangira, Sadifa Juma Hamisi na David Mbatia.
Hata hivyo, Mbatia ambaye awali alitambulishwa kuwa ni James Mbatia alienguliwa kutokana na kutokuwa na sifa na Sadifa kujitoa muda mfupi baada ya kujieleza mbele ya wajumbe wa Bunge hilo.
Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, Dk Kashililah na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad walimteua mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, Oliver Luena kuwa mwenyekiti msimamizi wa uchaguzi huo.
Uchaguzi huo ulioanza saa tisa alasiri hadi saa moja usiku, ulikabiliwa na changamoto kadhaa baada ya upigaji kura kuharibika kutokana na idadi ya wajumbe waliopiga kura kuongezeka kutoka 548 hadi 568 wakati wa kuhesabu.
Hali hiyo ilimlazimu Luena kuagiza uchaguzi huo urudiwe kauli ambayo ilizua mjadala mkali kwa baadhi ya wajumbe kupinga kurudiwa baadhi wakitaka urudiwe na wengine kupinga.
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alitaka uchaguzi huo usirudiwe kwa sababu hatua hiyo ingechukua muda mrefu bila sababu za msingi huku Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitaka uamuzi huo kufanywa kwa kura na Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe akitaka urudiwe. Mbunge wa Viti Maalumu, Sabrina Sungura (Chadema) alitaka kura tisa zilizozidi kugawanywa kwa wagombea watatu wa uenyekiti badala ya kurudia uchaguzi.
Katika ufafanuzi wake, Mbowe alisema uchaguzi huo ni wa kihistoria hivyo ni vyema ukarudiwa ili kuweka kumbukumbu sahihi za Bunge.
“Uchaguzi huu ni wa kihistoria, hivyo lazima urudiwe ili historia isije ikatuhukumu. Tuhakikishe waliopo ndani ya ukumbi ndiyo wanaopiga kura,” alisema Mbowe.

Kauli hiyo ya Mbowe iliungwa mkono na Luena ambaye alisema katika uchaguzi lazima idadi ya wajumbe iwiane na idadi ya kura zitakazopigwa.
Pamoja na ufafanuzi huo, kuliibuka majibizano mengine ya jinsi ya kurudia uchaguzi huo na Dk Kashililah alitangaza utaratibu wa wajumbe kufika mbele ya meza kuchukua karatasi za kupigia kura na wakati huohuo watakuwa wakihesabiwa idadi yao. Kazi hiyo ilichukua dakika 35.
Kuomba kura
Awali, wakati wagombea hao wakiomba kura, Kificho aliulizwa swali na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib Mnyaa kuhusu elimu yake lakini badala ya kujibu swali hilo alianza kueleza kuhusu madeni aliyonayo.
“Mheshimiwa Kificho umetueleza kuwa una uzoefu wa miaka 18 lakini hujatueleza kuhusu elimu yako, tungependa kufahamu kuhusu hilo,” alisema Mnyaa.
Akijibu swali hilo, Kificho alisema, “Kwa sasa sina takwimu kuhusu madeni yangu,” kabla ya kushtuka na kutaka kurudiwa kwa swali hilo.
Baada ya kulielewa swali hilo, Kificho alisema kuwa ana stashahada ya sheria ambayo aliipata katika chuo cha IDM Mzumbe ambacho hivi sasa ni Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mbunge wa Chakechake (CUF), Musa Haji Kombo alimuuliza Kificho: “Umetueleza uzoefu wako, sasa nauliza swali, kama nikikupigia kura utasikia raha?”
Katika majibu yake Kificho alisema, “Ndiyo maana tangu mwanzo niliwaomba kura za ndiyo.”
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mjumbe wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluochi kwa nyakati tofauti walisema kuwa ni wazi mazingira hadi ushindi wa Kificho yalikuwa yameandaliwa.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top