Maalim Seif
MOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar, umemtuhumu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwa ni kiongozi mwenye
viashiria vya udikteta.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alitoa kauli
hiyo juzi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Nungwi, Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Shaka alisema kitendo cha kiongozi huyo kukataa kuachia madaraka ya
kisiasa na kulipisha kundi la vijana ni udikteta usio na mipaka ndani
na nje ya Bara la Afrika.
Alibainisha kuwa inasikitisha kusikia kiongozi huyo akitangaza
kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika mwakani ilhali alishindwa mara nne katika chaguzi
zilizofanyika miaka iliyopita.
“Tangu mwaka 1992 hadi leo Maalim Seif ameshikilia vyeo ndani ya CUF,
amekuwa Makamu Mweyekiti wa CUF, mgombea urais wa kudumu, sasa Katibu
Mkuu na hataki kuachia ngazi ili kuwapa nafasi vijana, ndiyo maana
nasema ni dikteta hatari,” alisema.
Shaka aliongeza kuwa laiti Maalim Seif angelikuwa anaheshimu misingi
ya demokrasia na kutambua umri wake asingeendelea kushiriki siasa kama
alivyoahidi hivi karibuni kuwa hataacha siasa hadi aishiwe nguvu.
Shaka aliwataka vijana wa CUF kujiondoa katika chama hicho na
kujiunga CCM ili waweze kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wa kushikilia
nafasi za uongozi ambao sasa unahodhiwa na Maalim Seif.
“Tazameni CCM ilivyo, vijana tunapewa nafasi ili kuonyesha uwezo na
vipaji vyetu kisiasa, mkibaki huko hadi mtazeeka hamtapata nafasi ili
kuisaidia nchi yetu kimaendeleo,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM inaonyesha kuheshimu misingi ya demokrasia tangu
utawala wa TANU na ASP, ambapo kulikuwa na mabadiliko mbalimbali ya
viongozi wa ngazi za kisiasa na kiserikali, tofauti na vyama vingine
ikiwamo CUF.
Alitolea mfano kuwa kwa upande wa Jamhuri ya Muungnano aliondoka
madarakani Rais Julius Nyerere akampisha Ali Hassan Mwinyi ambaye
alimuachia kijiti Benjamin Mkapa na sasa taifa linaongozwa na Rais
Jakaya Kikwete.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, Rais wa Kwanza ni Abeid Aman Karume,
akafuatia Aboud Jumbe Mwinyi aliyempisha Idris Abdul Wakil, baadaye
Dk. Salmin Amour, akafuatia Dk. Amani Karume na sasa nchi inaongozwa na
Dk. Ali Mohamed Shein.
Shaka alilaumu utendaji aliouita ni legelege, usio wa uwajibikaji
na uadilifu kwa wizara ambazo ziko chini ya upinzani na kusema
waliopewa dhamana za madaraka hayo wameshindwa kutimiza wajibu wao
ipasavyo.
Aliitaja Wizara ya Afya chini ya Waziri Juma Duni Haji kwamba
haiwatendei haki wananchi huku katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mambo ya
utawala na utoaji wa huduma yakiendeshwa shaghalabaghala.
“Duni umepewa dhamana na Rais Shein ila hutimizi wajibu wako, hakuna
huduma za kuridhisha Mnazi Mmoja, wafanyakazi, wauguzi na waganga
wanalalamika, kutana nao, acha kuwakimbia,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment