Polisi wakiwa nje ya moja kati ya majengo yanayohisiwa kutumika kama
makazi ya mke na mume waliokamatwa Alhamisi kwa tuhuma za kujihusisha na
utumwa. Mmoja kati ya watuhumiwa hao ametokea Tanzania.
Mmoja kati ya watuhumiwa wawili
wanaoshutumiwa kuwashikilia wanawake watatu katika mazingira ya utumwa
kwa miaka 30 mjini London anatokea Tanzania, polisi Uingereza wamesema
Jumamosi.
Kamanda wa polisi wa London
Steve Roadhouse amesema watuhumiwa hao, ambao ni mke na mume wenye umri
wa miaka 67, ni wahamiaji waliokwenda London kwenye miaka ya 1960 kutoka
India na Tanzania.
Polisi wanahisi watuhumiwa
hao walikutanishwa na wanawake hao watatu katika “harakati za kisiasa”
zilizopelekea waanze kuishi “kijamaa” kwenye nyumba moja.
Haijulikani hali ilibadilika
vipi, lakini inaelekea kwenye miaka ya 1980, kibao kilibadilika, na
wanawake hao watatu wakajikuta wakigeuzwa vitwana wa timu hiyo ya mke na
mume.
“Tumeanza kuwachunguza
wahusika wote katika kikundi hiki cha kijamaa,” Kamanda Roadhouse
alisema mapema Jumamosi na kuongeza, “Tunatazama jinsi walivyofanya
kazi.”
Kesi hiyo ya utumwa ambayo
imezigusa nyoyo za mamilioni dunia nzima ilianza kurindima Oktoba 25
baada ya mmoja kati ya watumwa hao kupiga simu kituo cha wahisani
akiomba msaada, jambo lililopelekea polisi kuanzisha uchunguzi
uliofanikisha kuokolewa kwao.
Wanawake hao walioishi katika
mazingira ya utwana wa kutisha kwa miongo mitatu, ambao majina yao
hayajawekwa wazi, wanatokea Malaysia, Ireland na Uingereza. Taarifa ya
polisi inasema umri wa watumwa hao ni miaka 67, 57 na mdogo kabisa ni
mwanamama wa miaka 30.
Mke na mume waliokamatwa
Alhamisi katika sakata hili la utumwa walishawahi kunaswa katika mtego
wa polisi kwenye miaka ya 1970, ingawa polisi hawakuweka wazi walitenda
kosa gani.
Vilevile, wanahisiwa kuhusika
katika kile polisi walichokiita “makosa ya uhamiaji,” na katika kutoa
“huduma za kazi za shurti.” Wote wameachiwa kwa masharti hadi Januari
2014 huku uchunguzi ukiendelea.
0 comments:
Post a Comment