
WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kufufua karakana zote zilizokufa nchini.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi mameneja vitendea kazi
vyenye thamani ya zaidi sh milioni 800 vya karakana zote nchini
zilizopo chini ya TEMESA, alisema anashangazwa na mameneja hao kutoa
vibali vya magari ya serikali kwenda kutengenezwa katika gereji binafsi
huku wakidai mishahara serikalini.
Magufuli alisema kupatikana kwa vifaa hivyo kuwe mwisho wa kupeleka magari ya serikali kwenye gereji binafsi.
“Kupatikana kwa vifaa hivyo kutakuwa ni changamoto ya kila mhandisi
kutekeleza majukumu yake. Ninafahamu mnadai mamilioni katika taasisi za
serikali, hii ni changamoto kwetu serikalini. Magari yakiletwa katika
karakana zenu lazima kuwe na mikataba, na dereva lazima asaini
kitambulisho, ili wakichelewa kuwalipa madeni hayo taasisi hizo
zichukuliwe hatua,” alisema Magufuli.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Injinia Marcellin Magesa, alisema vitendea
kazi hivyo vilinunuliwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilikuwa
ni kwa ajili ya mikoa 10 ambayo ni Geita, Katavi, Njombe, Iringa,
Kilimanjaro, Tanga, Shinyanga, Kigoma, Rukwa na Pwani na tayari vifaa
hivyo vimeshasambazwa kwenye mikoa husika.
Alitaja baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa kwa awamu ya pili vimepelekwa
Dar es Salaam (Vingunguti), Dodoma, Tabora, Mbeya, Mtwara, Arusha,
Simiyu, Mara na Morogoro.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment